" SERIKALI YAAGIZA MALIPO YA WAFANYAKAZI YASHUGHULIKIWE NDANI YA WIKI MOJA

SERIKALI YAAGIZA MALIPO YA WAFANYAKAZI YASHUGHULIKIWE NDANI YA WIKI MOJA



Na Mapuli Kitina Misalaba 

Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi kwa vyombo vya habari nchini.

Akifungua rasmi Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji unaoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika Ukumbi wa New Generation jijini Dodoma, Mwinjuma ameielekeza TCRA kushirikiana na Bodi ya Ithibati kuhakikisha wafanyakazi wa vyombo vya habari wanalipwa stahiki zao kwa wakati, wakiwemo wale wanaodai mishahara ya zaidi ya miezi mitano.

Amesisitiza kuwa ndani ya wiki moja anatarajia kupokea mrejesho wa hatua zilizochukuliwa kuhusu suala hilo.

Katika hatua nyingine, Mwinjuma amesema Serikali imepunguza ada za maombi ya leseni kwa vyombo vya habari mtandaoni kutoka shilingi laki tano hadi elfu 50, huku ada ya maombi ikiwa ni shilingi elfu 10 tu, hatua inayolenga kutoa fursa zaidi kwa wadau kushiriki katika sekta hiyo.

Amesisitiza umuhimu wa ubora wa maudhui yanayorushwa na vyombo vya utangazaji kwa kuzingatia maadili ya taaluma pamoja na kulinda haki miliki. Amesema haki ya kupata taarifa ni ya kila Mtanzania, hivyo vyombo vya habari vinapaswa kuwafikia wananchi wote bila upendeleo.

Aidha, amesema wizara hiyo itaendelea kuboresha mazingira ya sekta hiyo ili kuhakikisha wananchi wa vijijini wanapata huduma za utangazaji kwa urahisi, sambamba na kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa ikiwemo Akili Unde (AI) kwa matokeo chanya.
Mwinjuma pia ameielekeza Kampuni ya Usambazaji wa Machapisho na Vifaa vya Utangazaji (KOSOTO) kushirikiana na TCRA kupambana na waharamia wa maudhui, na kuwasilisha mrejesho ndani ya mwezi mmoja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari, ametaja takwimu za vyombo vya habari vilivyosajiliwa nchini na kuahidi kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuboresha miundombinu ya mawasiliano kwa kuzingatia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Viongozi na wadau wakiwemo wawakilishi wa vyama mbalimbali vya vyombo vya habari wamewasilisha taarifa zao na kushiriki katika meza za majadiliano, huku mada mbalimbali zikiendelea kujadiliwa.

Mkutano huo unaendelea kwa siku mbili, Februari 12 na 13, 2026, ukiwakutanisha wadau kujadili namna ya kuimarisha na kupanua huduma za utangazaji nchini.

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post