
Na Mwandishi Wetu, Siha – Kilimanjaro
Mnamo Februari 10, 2026, mbele ya Mhe. Jasmin A.A katika Mahakama ya Wilaya ya Siha, TAKUKURU (W) Siha ilifungua mashauri matatu ya Uhujumu Uchumi namba 2831, 2834 na 2837 ya mwaka 2026, kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhidi ya Dkt. Donatus Boniphace Tsete, Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma katika Hospitali ya Taifa ya Kibong’oto iliyopo Wilaya ya Siha.
Mshtakiwa anakabiliwa na jumla ya makosa saba katika kila shauri. Katika kosa la kwanza, anashtakiwa kwa matumizi mabaya ya mamlaka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007, kikisomwa pamoja na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza, kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200 (marejeo ya mwaka 2019). Inadaiwa kuwa, kwa kutumia cheo chake, alifuja fedha zilizotengwa kwa ajili ya mafunzo ya usimamizi wa wagonjwa wa kifua kikuu sugu (Drug-Resistant Tuberculosis Mentorship) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Same (Tsh 5,082,000/=), Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro (Tsh 5,061,000/=) na Halmashauri ya Wilaya ya Arusha (Tsh 5,490,000/=), katika kesi tatu tofauti.
Kosa la pili ni kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335(1) na 337 vya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 (marejeo ya mwaka 2022), kwa madai ya kughushi saini katika orodha ya mahudhurio (attendance) kuonesha kuwa washiriki wa mafunzo walisaini na kulipwa fedha hizo.
Kosa la tatu ni kuandaa nyaraka zenye maelezo ya uongo kinyume na vifungu vya 342 na 337 vya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 (marejeo ya mwaka 2022). Nyaraka hizo ni hati za malipo na viambatisho vyake, ikiwemo dokezo sabili na orodha ya malipo (pay list).
Kosa la nne ni kutumia nyaraka hizo kumdanganya mwajiri, kinyume na kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 (R.E 2019).
Kosa la tano ni ubadhirifu wa fedha jumla ya Tsh 15,633,000/= kinyume na kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.
Kosa la sita ni kuisababishia mamlaka hasara ya Tsh 15,633,000/= kinyume na Aya ya 21 ya Jedwali la Kwanza, kifungu cha 57(1) na 60(2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200 (toleo la mwaka 2019).
Kosa la saba ni kuwasilisha nyaraka zenye maelezo ya uongo kinyume na vifungu vya 342 na 337 vya Kanuni za Adhabu, Sura ya 16 (toleo la mwaka 2019).
Mshtakiwa amekana mashtaka yote na amekidhi masharti ya dhamana yaliyowekwa na Mahakama, hivyo yupo nje kwa dhamana. Kesi imeahirishwa hadi Februari 23, 2026.
Katika hatua nyingine, mshtakiwa ameiomba Mahakama ruhusa ya kufanya majadiliano ya kukiri kosa (plea bargaining) katika mashauri yote matatu. Ameelekezwa kuandika barua kwa Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Kilimanjaro kuhusu ombi hilo, na tayari amewasilisha barua hiyo akisubiri majibu.
Mashauri hayo yanaendeshwa na mawakili wa Serikali, Bi. Suzan Kimaro na Bw. Bernard Ndamallya kutoka TAKUKURU.
TAKUKURU Siha – Kilimanjaro, Februari 10, 2026
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment