" Askofu Bagonza Atoa Onyo

Askofu Bagonza Atoa Onyo

 

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dkt. Benson Bagonza, ametoa wito kwa Watanzania “kuomboleza vizuri” kifo cha Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, huku akionya dhidi ya majaribio ya kuitenganisha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na kiongozi huyo au kuwagawa Wakristo nchini.

Kupitia ujumbe wake wa rambirambi aliouchapisha mtandaoni, Askofu Bagonza amemuelezea Hayati Kardinali Pengo kama “Jabali la Maadili ya Kanisa” na kiongozi wa kijamii aliyekuwa tayari kutoa mawazo yake kwa ajili ya ustawi wa taifa wakati wote.

Askofu Bagonza ametoa msisitizo kuwa Mwadhama Pengo na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ni kitu kimoja kinachoshirikiana, hivyo ni makosa kwa mtu yeyote kujifanya anampenda Pengo huku akiichukia au kuishambulia TEC.

“Mwadhama Pengo na TEC havitenganishwi. Huwezi kumpenda Pengo ukaichukia TEC au kinyume chake. Tumia hekima kama huna akili ya kutumia. Kanisa Katoliki limeumizwa na wasioujua muundo wake. Kwenye msiba huu ‘vijora viwe likizo’, asiyependa kuomboleza, awape nafasi wanaoomboleza”, amesisitiza Askofu Bagonza.

Katika kile kinachoonekana kama kujibu mijadala ya kisiasa na kijamii, Askofu amewataka watu kuacha kubuni msimamo wa mwisho wa Kardinali Pengo au “kummiliki” kifikra. Amesema hali yake na Muumba wake ni jambo la siri, na wajibu wa waliobaki ni kumuombea na si kumpangia mawazo ambayo hakuyaeleza.

“Mwadhama Pengo ni bingwa wa maadili ya kiroho. Kama hukuwa naye siku za mwisho, usikimbilie kubuni alikuwa anawaza nini. Hali yake na msimamo wake wa mwisho anaujua yeye na Muumba wake. Letu ni kumuombea, si kummiliki”, ameeleza.

Askofu Bagonza amekumbusha kuwa Kardinali Pengo amefanya kazi na Marais wote sita (6) wa Tanzania na kuona mengi. Amesisitiza kuwa viongozi wa kisiasa, wawe wema au wabaya, ni watu wa kupita, lakini taasisi ya Kanisa itabaki imara daima.

Ujumbe huo pia umegusia umuhimu wa umoja kati ya madhehebu mbalimbali ya Kikristo (TEC, CCT, PCT, SDA nk) na mshikamano wa kidini kati ya Wakristo na Waislamu nchini Tanzania. Amesema Kardinali Pengo alikuwa mpinzani wa dhana ya “Dini ya Taifa” na aliamini katika Tanzania ya wote, bila kujali tofauti za mavazi..

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post