" ASKOFU SANGU APOKEA MICHE 100,AHIMIZA UTUNZAJI WA MAZINGIRA NA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN

ASKOFU SANGU APOKEA MICHE 100,AHIMIZA UTUNZAJI WA MAZINGIRA NA KUUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN

Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, Mhashamu Liberatus Sangu, amepokea miche  100 ya miti ya matunda, mbao na kivuli kutoka  taasisi ya Joseph Muhunda Nyerere Foundation kwa lengo la kuendeleza juhudi za utunzaji wa mazingira

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya miche hiyo, Askofu  Sangu amepongeza  hatua  hiyo na kusema  kuwa  ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kitaifa za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amepongeza hatua hiyo  na kubainisha kuwa utunzaji wa mazingira ni wajibu wa kila mmoja, na kwamba  ni hatua  nyingine katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, za kuhimiza uhifadhi wa mazingira nchini.

Aidha, Askofu Sangu amesema kuwa juhudi hizo zinaendana na mafundisho ya hayati Baba Mtakatifu  Fransisko, ambaye  enzi za uhai wake alikuwa akisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira kama sehemu ya kushiriki katika uumbaji wa Mungu

Amesema pamoja na kulinda mazingira, ni muhimu pia taasisi hiyo ikajikita  katika  juhudi za kudumisha amani, kuipenda nchi yao na kuwa wazalendo wa kweli.

Kwa upande wake, Mkurugenzi  wa  Taasisi  hiyo  Joseph Muhunda Nyerere  amesema amepokea maelekezo hayo na kuahidi kuyazingatia. ameeleza kuwa ataendelea kuhamasisha jamii  kuishi kwa kuzingatia misingi ya amani, uzalendo na uwajibikaji sambamba na kuendeleza kampeni za uhifadhi wa mazingira nchini.

Taasisi ya JOSEPH MUHUNDA NYERERE FOUNDATION inajihusisha na masuala ya uhifadhi wa mazingira Nchini.




Post a Comment

Previous Post Next Post