" BILIONI 79 KUSHUSHWA KUIMARISHA ULINZI: VITUO VYA POLISI 698 KUJENGWA NCHI NZIMA

BILIONI 79 KUSHUSHWA KUIMARISHA ULINZI: VITUO VYA POLISI 698 KUJENGWA NCHI NZIMA



Serikali imetangaza mpango mkambe wa kuimarisha usalama wa raia na mali zao nchini kwa kutenga zaidi ya Shilingi bilioni 79 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya polisi 698 katika maeneo mbalimbali. 

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuhakikisha huduma za ulinzi zinawafikia wananchi kwa ukaribu zaidi na kukabiliana na changamoto za uhalifu katika maeneo yanayokua kwa kasi.

Akibainisha ukubwa wa mradi huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohamed Mahmoud, amesema kuwa uwekezaji huo mkubwa katika miundombinu ya Jeshi la Polisi ni kielelezo cha dhamira ya Serikali ya kuweka mazingira rafiki ya usalama yanayochochea shughuli za maendeleo. 

Naibu Waziri Mahmoud ametoa maelezo hayo wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa vituo vya polisi katika Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu ya kikazi visiwani Unguja.

Katika ukaguzi huo wa miundombinu ya jeshi hilo, Naibu Waziri amesisitiza kuwa kukamilika kwa vituo hivyo kutaongeza ufanisi wa utendaji kazi wa askari na kurejesha imani ya wananchi kwa vyombo vya dola. 

Amesema kuwa ujenzi huo utazingatia viwango vya kisasa ili kuendana na mahitaji ya sasa ya kiulinzi, huku akitoa wito kwa wakandarasi na wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana katika majengo yote yatakayojengwa nchi nzima.

Mradi huu unatarajiwa kuwa mkombozi kwa maeneo mengi ambayo hapo awali yalikuwa yakikabiliwa na upungufu wa vituo vya polisi, hali iliyokuwa ikiwalazimu wananchi kufuata huduma za usalama umbali mrefu. 

Kwa kuanza na ukaguzi huo visiwani Unguja, Serikali inatuma ujumbe wa wazi kuwa uimarishaji wa ulinzi ni kipaumbele cha kitaifa kinachogusa pande zote mbili za Muungano kwa ajili ya utulivu wa kudumu wa Watanzania.

MWISHO

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post