Na Lydia Lugakila
Mbeya.
Diwani wa Kata ya Iwambi Jijini Mbeya, Gloria Ipopo Mwamajemba (Mchina), amemshukuru na kumpongeza Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari Iwambi, Nahadel Mohammed, kwa kujitolea kuchimba kisima cha maji cha kisasa shuleni hapo ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji.
Muda mfupi baada ya shule hiyo kupandishwa hadhi na kuanza Kidato cha tano na sita, mahitaji ya maji yameongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti huyo ambaye pia ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Mbeya, alichukua hatua ya haraka kwa kuwapeleka wataalamu kufanya upimaji wa eneo la kuchimba kisima.
Hatimaye, mtambo wa kisasa wa kuchimba kisima umefika na kazi imeanza rasmi.
Mbali na kugharamia uchimbaji wa kisima kwa asilimia 100 kwa fedha zake binafsi, Nahadel Mohammed pia ametoa fedha kwa ajili ya kuezekea jiko la wanafunzi kwa zege imara litakalotumika kubeba matanki ya kuhifadhia maji.
Aidha, amejitolea kuleta matanki mawili ya maji yenye uwezo wa lita 5,000 kila moja ili kuhakikisha upatikanaji wa maji unakuwa wa uhakika.
Akizungumza na wanafunzi, Mwenyekiti huyo aliwahimiza kusoma kwa bidii akisisitiza kuwa wao ni viongozi wa baadaye.
Pia aliwasihi kutunza miundombinu ya maji inayojengwa kwa ushirikiano kati ya serikali na wadau ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Aliwataka kuwa wazalendo na kuendelea kudumisha amani nchini, huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu na namna anavyoijali Kata ya Iwambi.
Katika kuonesha kugusa maisha ya wanafunzi mmoja mmoja, Mwenyekiti huyo pia alitoa msaada wa fedha kwa mwanafunzi mwenye mahitaji maalum aitwaye Chester Philimone ili aweze kujikimu katika masomo yake.
Kwa upande wake, Diwani Grolia Ipopo Mwamahemba alisema zawadi pekee wanayoweza kumpa Mwenyekiti huyo ni wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa na kutokomeza sifuri.
Aidha, aliwataka wadau wengine kujitokeza kuisaidia Kata ya Iwambi kwani bado kuna mahitaji mengi ikiwemo ujenzi wa maktaba ya shule, upatikanaji wa vifaa vya TEHAMA na kuboresha miundombinu mingine ya elimu.
Diwani huyo pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake thabiti unaowavutia wadau mbalimbali kuendelea kuleta maendeleo katika Kata ya Iwambi.

Post a Comment