Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dkt.Festo Dugange, ameipongeza Kampuni ya KADERES Peasant Development Public Limited Company kwa dhamira yake ya dhati ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia kilimo chenye tija kinachozingatia utunzaji wa mazingira.
Naibu Waziri Dkt.Dugange ametoa pongezi hizo Februari 26, 2026, alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua Mradi wa Shamba Darasa la Kinoni Agroforest unaomilikiwa na kampuni hiyo, uliopo Kata ya Ndama, Wilaya ya Karagwe, mkoani Kagera.
Akizungumza katika ziara hiyo, amesema uwekezaji huo ni mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali katika kukuza kilimo mseto kinachoongeza kipato kwa wakulima huku kikihifadhi mazingira. Aidha, amempongeza Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bw. Leonard Kachebonaho, kwa kuanzisha mtandao wa wakulima unaowawezesha kunufaika na biashara ya hewa ukaa.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo, Afisa Kilimo wa KADERES, Bw. Mchunguzi Karabamu, amesema shamba hilo la mfano lenye ukubwa wa hekari 58 limeanzishwa kwa lengo la kubadilisha mtazamo wa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya ardhi, kuhamasisha kilimo chenye tija na uzalishaji endelevu, pamoja na kutoa mafunzo kwa vitendo juu ya namna ya kuzalisha mazao ya chakula na biashara hata katika maeneo yenye milima na mawe.
Ameongeza kuwa mradi huo unatoa ajira kwa jamii inayozunguka shamba, unahamasisha utunzaji wa mazingira na kufundisha kilimo kinachohifadhi rutuba ya udongo kupitia matumizi ya mazao funika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Bw. Leonard Kachebonaho, amesema zaidi ya wakulima 2,000 tayari wananufaika kwa kupokea malipo kupitia biashara ya hewa ukaa, huku zaidi ya wakulima 136,000 wakiwa wamesajiliwa kuanza kunufaika na mpango huo katika mikoa mbalimbali nchini.
Amebainisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 3 tayari zimelipwa kwa wakulima kupitia biashara hiyo. Aidha, kampuni hiyo ipo katika mazungumzo na CRDB Bank Plc, ambayo inatarajia kutoa takribani shilingi bilioni 9 kwa ajili ya kuwezesha usajili wa wakulima milioni 1.5 kutoka mikoa ya Kagera, Mbeya, Kigoma, Geita na Katavi.
Miongoni mwa wanufaika wa mradi wa hewa Ukaa ,Bw.Enock Gabagambi mkazi wa Kata ya Nyakahanga, Aloyce Bagambilana mkazi wa Rugera pamoja na Bw. Dauson Beyeza mkazi wa Kata ya Kamagambo, wamesema kuna mabadiliko makubwa ya kiuchumi kabla na baada ya kuanza kupokea malipo ya hewa ukaa.
Wamesema mradi huo ni chachu ya mapinduzi ya uchumi kwani unachangia , kuongeza kipato cha wakulima na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mazao yanayolimwa katika shamba hilo ni pamoja na kahawa aina ya Arabika na Robusta, mdalasini, mikarafuu, migomba, nanasi, parachichi, fenesi, michenza, miembe na mipera. Hadi sasa, mradi huo umegharimu jumla ya shilingi milioni 700,650,000.






Post a Comment