" EMEDO YATANGAZA UJIO WA TUZO ZA WANAHABARI WANAOHAMASISHA USALAMA MAJINI

EMEDO YATANGAZA UJIO WA TUZO ZA WANAHABARI WANAOHAMASISHA USALAMA MAJINI

 

Na Tonny Alphonce-Misalaba Media

Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO) kupitia mradi wake wa Kuzuia Kuzama Maji Ziwa Victoria limetangaza ujio wa tuzo za waandishi wa habari zinazohamasisha usalama majini.

Akizungumza na Waandishi wa habari mjumbe wa bodi ya EMEDO na mratibu wa tuzo hizo Edwin Soko amesema lengo la tuzo hizo ni kutambua mchango wa waandishi wa habari lakini pia  kuwahamasisha kuandika habari nyingi zinazoihamasisha jamii juu ya usalama wao wawapo majini.

Soko amesema tuzo hizo Kwa mara ya kwanza zitatolewa katikati ya mwaka huu 2026 zikihusisha habari zote zinazohamasisha usalama majini kwa mwaka mmoja uliopita.

Akizungumzia baadhi ya vigezo vitakavyoamua washindi Soko amesema habari lazima ilete mabadiliko katika Jamii,habari iwe imejikita kwenye utafiti,habari ilete suluhisho la changamoto iliyopo,habari iwe na vyanzo vyote  muhimu pia habari iwe na takwimu zinazotambulika.

Soko amesema tuzo hizo zitakuwa na washindi katika maeneo matatu,Mshindi wa kwanza,mshindi wa pili na mshindi wa tatu.

"Tunaangalia uwezekano wa kutoa zawadi kwenye vyombo vyote vya habari, Traditional Media na Modern Media"alisema Soko.

Upande wa zawadi Soko amesema washindi watapata zawadi ya Camera za kisasa, Laptop za kisasa pamoja na zawadi zingine ambazo zitaendana na kazi wanazofanya waandishi wa habari hapa nchini.

Kwa upande wake Meneja mradi wa Kuzuia Kuzama Maji Ziwa Victoria,Arthur Mgema amesema hadi sasa vyombo vya habari vimechangia Kwa kiasi kikubwa kuutambulisha mradi wa Kuzuia Kuzama Maji Ziwa Victoria na kubadili tabia za wavuvi na wanajamii wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Victoria.

Mgema pia amewapongeza waandishi vinara wa habari zinazohamasisha usalama majini Kwa kuendelea kutoa elimu Kwa Jamii na mabadiliko yameanza kuonekana hasa upande wa wavuvi na watumiaji wa vyombo vya majini kuona umuhimu wa kuvaa maboya Kila wanapoingia majini.

Mgema amesema kupitia tuzo hizo anaamini waandishi wa habari wataibua changamoto zinazosababisha ajali majini,wataibua pia Fursa zilizopo kwenye vyanzo vyetu vya maji na hatimaye kupunguza vifo vinavyotokea majini.

 



Post a Comment

Previous Post Next Post