" FCT YAWAJENGEA UWEZO WAFANYABIASHARA NA WATUMIAJI KIGOMA KUHUSU HAKI ZA USHINDANI

FCT YAWAJENGEA UWEZO WAFANYABIASHARA NA WATUMIAJI KIGOMA KUHUSU HAKI ZA USHINDANI

KIGOMA

Baraza la Ushindani(FCT), moja ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, imeendesha kikao cha kuwajengea uwezo watumiaji wa huduma, wadau na wafanyabiashara wa Mkoa wa Kigoma kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu haki za ushindani na taratibu za rufaa.

Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa Lake Tanganyika Hotel na kuhudhuriwa na wadau kutoka sekta mbalimbali za biashara na huduma.

Akifungua kikao hicho, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Ndg. Deogratias Sangu, aliwataka wananchi kutumia elimu waliyoipata kuelewa haki zao katika ushindani na udhibiti wa soko. Alisema uelewa wa sheria na taratibu za ushindani utasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima, kuimarisha uwajibikaji wa taasisi na kujenga mazingira ya Soko yenye usawa na haki.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa FCT, Mhe. Jaji Rose Ally Ebrahim, alisema Baraza lina jukumu la kusikiliza na kuamua rufaa zinazotokana na maamuzi ya Fair Competition Commission (FCC) pamoja na mamlaka za udhibiti wa sekta mbalimbali ikiwemo LATRA, EWURA, TCRA, TCAA na PURA.

Aliwahimiza wananchi wa Kigoma kulitumia Baraza hilo wanapokuwa hawajaridhishwa na maamuzi ya vyombo husika, akisisitiza kuwa mfumo wa rufaa umewekwa kisheria ili kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati na kwa uwazi.

“Watu wakijua wapi pa kupata haki, wanapunguza gharama za kuhangaika kutoka sehemu moja ya huduma hadi nyingine,” alisema Mhe. Jaji Ebrahim, akisisitiza kuwa elimu ya sheria ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wananchi na wafanyabiashara kukua kiuchumi.

Wadau waliohudhuria kikao hicho waliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kuimarisha taasisi zinazolinda na kusimamia haki za wafanyabiashara na watumiaji wa huduma.

Walisema juhudi hizo zinaonyesha dhamira ya Serikali ya kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi kupitia mfumo wa ushindani ulio wazi, shindani na wa haki, unaochochea ukuaji wa biashara na ustawi wa taifa.

     

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post