

Jeshi la Polisi linapenda kujulisha kuwa, linaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi kama yalivyoainishwa na Sheria za nchi. Utekelezaji huo unakwenda sambamba na kushirikiana na wananchi katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu jambo ambalo limepelekea nchi yetu kuendelea kuwa shwari.
Pamoja na ushwari huo yapo matukio machache ambayo yametokea na yameendelea kufanyiwa kazi na baadhi ya watuhumiwa wameendelea kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kufikishwa mahakamani kama ambavyo Makamanda wa Polisi wa Mikoa wamekuwa wakitoa taarifa kila mara kupitia Vyombo vya Habari.
Aidha, kupitia mitandao ya kijamii, kumejitokeza baadhi ya watu kuendeleza tabia za kuhamasisha wananchi wajiingize kwenye vitendo vya kihalifu na baadhi wameshawishika na kujiingiza kwenye uhalifu wa kimtandao na baadhi wameshakamatwa na wengine wanaendelea kutafutwa.
Baadhi ya watu hao wanaoshawishi uhalifu huo ni pamoja na anayejitambulisha au wanaojitambulisha kwa jina la TFF na kutoa taarifa mbalimbali kuwa, wanafanya mazoezi porini na kwamba wameshafanya matukio kadhaa ya kijinai. Jeshi la Polisi linakanusha taarifa wanazosambaza kuwa kikundi chao kimetenda uhalifu huu na ule kwani si za kweli.
Jeshi la Polisi linapenda kuwahakikishia wananchi kuwa, linawafuatilia kwa karibu sana watu hao pamoja na matamshi na jumbe zao wanazotengeneza na kusambaza kwa lengo la kuleta taharuki kwa wananchi.
Ufuatiliaji unafanyika usiku na mchana hivyo wananchi muondoe hofu na endeleeni na shughuli zenu za kiuchumi na kijamii kama kawaida.
Aidha, Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi kuendelea kuwapuuza watu hao na wengineo pamoja na taarifa na jumbe zao kwani hawapo ndani ya mipaka ya nchi na hata wanacho hamasisha hawatashiriki na hawatakuwa na uwezo wala mwanya wa kuwaruhusu kushiriki.
Wananchi watambue lengo la watu hao ni kutaka kutuchonganisha, kutujengea chuki ili tuhamasike tujiingize kwenye uhalifu na vitendo vya vurugu.
Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua yeyote yule atakaye endelea kujihusisha na vitendo kama hivyo au kujiingiza katika uhalifu wa aina yeyote ile kwani ni kinyume na sheria.
Imetolewa na;
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi
Dodoma,Tanzania
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment