Na Fabius Clavery Misalaba Media-Kagera.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Mhe. Devotha Daniel, ametoa msaada wa shilingi milioni moja kwa ajili ya matibabu ya mtoto Grecseous Raphael (miezi 4), mkazi wa Kata ya Kihanga, Wilaya ya Karagwe, anayesumbuliwa na uvimbe kichwani, ili kumwezesha kufikishwa katika Hospitali ya Kanda ya Bugando kwa ajili ya upasuaji.
Msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ukiwa na lengo la kuendelea kusambaza tabasamu na matumaini kwa wananchi wenye uhitaji maalum. Mbali na fedha taslimu, Mhe. Devotha ameahidi kugharamia bima ya afya kwa familia nzima ya mtoto huyo, hatua inayolenga kuhakikisha wanapata huduma za matibabu kwa urahisi pindi wanapohitaji.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mhe. Devotha amesema alipata taarifa za mtoto huyo kupitia matangazo ya kituo cha redio ya jamii cha Fadeco Radio, ambapo mama wa mtoto alikuwa akiomba msaada kwa wasamaria wema. Alisema baada ya kusikia taarifa hizo aliguswa na kuamua kufika moja kwa moja katika familia hiyo ili kujionea hali halisi na kutoa mchango wake.
Aidha, Mbunge huyo amesema hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na ulinzi wa matibabu. Amesisitiza kuwa uongozi ni kuwagusa wananchi kwa vitendo na kusimama nao hasa wanapopitia changamoto.
Kwa upande wake, mama wa mtoto huyo, Bi. Swaumati Silaji, amemshukuru Mbunge huyo kwa kufika nyumbani kwao, kuwafariji na kutoa msaada huo . Amesema msaada huo umewarejeshea matumaini mapya ya kumuona mtoto wao akipona na kurejea katika hali ya kawaida.
Vilevile Wameahidi kuendelea kumuombea Mbunge huyo ili aendelee kuwahudumia wananchi kwa moyo wa huruma na kujitoa.
Naye Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Karagwe, Georgiana Mkapapa, amesema kitendo hicho kinaonesha namna Mbunge huyo alivyo karibu na wananchi wake. Amewataka wanawake na wananchi kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono katika jitihada zake za kuwatumikia na kuwaletea maendeleo.
Katika ziara hiyo, Mhe. Devotha aliambatana na Katibu wake, Katibu wa UWT Karagwe pamoja na Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Karagwe, wakionesha mshikamano wa pamoja katika kuwatumikia wananchi wa Mkoa wa Kagera.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment