" KANALI KIDO ATANGAZA MKAKATI WA ULINZI NI KIPAUMBELE NAMBA MOJA KAGERA

KANALI KIDO ATANGAZA MKAKATI WA ULINZI NI KIPAUMBELE NAMBA MOJA KAGERA


Na Fabius Clavery -Misalaba Media-Kagera.

‎Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Kanali Yahya Ramadhani Kido, ametangaza rasmi kuwa eneo la ulinzi na usalama litakuwa kipaumbele namba moja katika kipindi chake cha uongozi mkoani humo.

‎Kanali Kido ameyasema hayo Februari 13, 2026 wakati wa hafla ya kukabidhiwa ofisi kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatuma Mwassa. Katika hotuba yake, ameainisha wazi maeneo atakayoyapa kipaumbele katika kuendeleza Mkoa wa Kagera, akisisitiza kuwa ulinzi na usalama ni msingi wa maendeleo.

‎Amesema maendeleo hayawezi kupatikana bila amani na utulivu, hivyo ameahidi kusimamia kwa karibu masuala ya kiusalama ili kuhakikisha Kagera inaendelea kuwa mahali salama kwa wananchi na wawekezaji.

‎Aidha, Kanali Kido ameweka mkazo katika usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa ni lazima miradi ikamilike kwa wakati, kwa viwango vinavyotakiwa na kwa kuzingatia thamani ya fedha za umma. Ameeleza kuwa yuko tayari kushirikiana na wadau wote kwa lengo la kuwaletea manufaa wananchi wa Kagera.

‎Kwa upande wake, Fatuma Mwassa akizungumza katika hafla hiyo, amemuomba Mkuu huyo mpya wa Mkoa kuendelea kusimamia miradi yote ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa, ikiwemo barabara za kimkakati. Pia ameeleza kuwa mkoa uliweka mkakati wa kuhakikisha halmashauri zake zinazalisha ajira kwa vijana ili kuwainua kiuchumi.

‎Kadhalika, amebainisha juhudi zinazoendelea za kukuza uchumi wa kila mwanakagera kupitia kilimo cha zao la kahawa, pamoja na kuendeleza Tamasha la Ijuka Omuka linalolenga kuhamasisha wazawa wa Kagera kurejea nyumbani na kuwekeza mkoani humo kwa ajili ya kuinua uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla.

‎Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM taifa, Mkoa wa Kagera, Kareem Amri, amesisitiza kuwa chama kitaendelea kuwa nguzo muhimu katika kusukuma mbele ajenda za maendeleo mkoani humo. Ameeleza kuwa CCM itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mkoa kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa ufanisi na changamoto za wananchi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati, huku akihimiza mshikamano wa viongozi na wananchi katika kulinda amani na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment

Previous Post Next Post