" DKT. MWIGULU AAGIZA TAKUKURU ICHUNGUZE MIANYA YA WIZI

DKT. MWIGULU AAGIZA TAKUKURU ICHUNGUZE MIANYA YA WIZI






*Ataka uchunguzi ununuzi wa vifaa vya ujenzi hospitali ya Wilaya Kilindi

Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amemwagiza Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, Bw. Ramadhani Ndwatah afuatilie suala la gharama ya miradi kuongezeka na saruji kuganda kwa kisingizio cha kununuliwa kutoka mbali ili kubaini kama kuna mianya ya wizi.

“Kamanda wa TAKUKURU fanyia kazi hili eneo, hiki kichaka cha gharama kuongezeka kwa sababu ya umbali kinazidi kukua. Wanaomba nyongeza ya fedha wakati ilishatolewa yote. Hatuwezi kupoteza juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutafuta fedha za miradi halafu ninyi mnakuja kuzichezea,” amesema.

Ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Februari 14, 2026) wakati akizungumza na wananchi wa Kilindi mara baada ya kuweka jiwe la msingi la Hospitali ya Wilaya Kilindi iliyojengwa kwa gharama ya sh. bilioni 2.64.

Waziri Mkuu amesema kuna michezo inachezwa na watumishi wa umma ili kuhalalisha upotevu wa fedha ambapo watumishi wanadai kuwa vifaa vinaagizwa kutoka mbali. “Jana nikiwa Handeni nilisema kuhusu ujenzi wa VETA ambao umekwama kwa sababu mifuko ya saruji zaidi ya 1,200 imeganda. Tanga kuna kiwanda cha saruji lakini wao wananunua kutoka Dar es Salaam na Mbeya. Kuna miradi inajengwa Njombe nao wananunua saruji Dar es Salaam badala ya Mbeya ambako ni jirani zaidi. Kamanda fuatilia, nipate taarifa haraka.”

Akielezea ujenzi wa hospitali hiyo, Waziri Mkuu amesema hospitali hiyo inatakiwa iwe na hadhi ya Mkoa ili ijitegemee kwani mgonjwa akipata dharura atapaswa kupelekwa Tanga mjini ambako ni mbali. Kilindi iko umbali wa kilometa 219 kutoka Tanga mjini.

Waziri Mkuu amesema ameridhishwa na ubora wa majengo katika hospitali hiyo, lakini akahoji ni kwa nini kuna upungufu wa majengo ikilinganishwa na idadi ya majengo tisa yaliyokuwa yamebajetiwa tangu awali.

“Majengo yaliyopo ni machache kuliko yaliyokusudiwa ikiwa fedha yote ya utekelezaji wa mradi ilitoka. Majengo yapo kwenye viwango vizuri, ila fedha iliyokuja ilikuwa ijenge majengo mengi zaidi lakini mmejenga pungufu, fedha nyingine ipo wapi? Michezo ya upotevu wa fedha za Serikali hatuwezi kuivumilia”

Alipoulizwa ni kwa nini idadi ya majengo haijatimia, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, Bw. Kulwa Mgalula alisema walishindwa kupata majengo yote tisa kwa sababu gharama za manunuzi ziliongezeka kutokana na umbali wa eneo hilo.

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Pendo Mang’ombe alisema gharama za mradi hadi sasa ni sh. bilioni 2.64 ambapo kati ya fedha hizo sh. bilioni 2.51 zimetoka Serikali Kuu, sh. milioni 50 ni za mapato ya ndani ya Halmashauri na sh. milioni 89.9 zimetoka Benki ya Dunia.

Alisema ujenzi wa hospitali hiyo umesaidia kuwapunguzia wananchi adha na gharama kubwa za matibabu ambazo walilazimika kuzifuata katika wilaya za jirani.

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254




Post a Comment

Previous Post Next Post