" RAIS SAMIA ASISITIZA UMUHIMU WA NCHI ZA AFRIKA KUPUNGUZA UTEGEMEZI MISAADA YA NJE

RAIS SAMIA ASISITIZA UMUHIMU WA NCHI ZA AFRIKA KUPUNGUZA UTEGEMEZI MISAADA YA NJE



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wanahabari juu ya ufadhili endelevu wa kutokomeza Malaria pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika, tarehe 14 Februari, 2026 jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Mkutano huo na Wanahabari ulikuwa chini ya Mwenyekiti wa Umoja wa Viongozi wa Afrika dhidi ya Malaria (ALMA) Rais wa Botswana Mheshimiwa Duma Gideon Boko.

…………..

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameshiriki mkutano wa ngazi ya juu na vyombo vya habari uliojadili ufadhili endelevu wa mapambano dhidi ya malaria barani Afrika, pembezoni mwa Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaofanyika katika Makao Makuu ya Umoja huo jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Akizungumza katika mkutano huo ulioandaliwa na AU kwa kushirikiana na African Leaders Malaria Alliance (ALMA), Rais Dkt. Samia alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuimarisha ufadhili wa ndani wa programu za malaria, kupunguza utegemezi wa misaada ya nje, pamoja na kuimarisha mifumo ya afya.

Alieleza kuwa mapambano dhidi ya malaria yanahitaji uongozi thabiti wa Waafrika wenyewe, umiliki wa kweli wa programu zake na dhamira ya kisiasa ya muda mrefu, akibainisha kuwa vita dhidi ya malaria si suala la afya pekee bali pia ni ajenda ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa rasilimali watu.

Rais Samia alitaja uzoefu wa Tanzania katika mapambano hayo, akisema nchi ni miongoni mwa vinara wa ajenda ya kutokomeza malaria barani Afrika na mwenyeji wa taasisi ya ALMA, hatua inayochangia kuratibu mifumo ya uwajibikaji na utekelezaji unaolenga matokeo.

Aidha, alieleza kuwa Tanzania imewekeza katika tafiti za kisayansi na ubunifu kupitia Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), ikiwemo maendeleo ya teknolojia za kisasa za kudhibiti maambukizi ya malaria, matumizi ya vyandarua, chanjo, pamoja na kuboresha mifumo ya matibabu na ufuatiliaji wa wagonjwa.

Aliongeza kuwa Serikali imeunganisha afua za malaria katika huduma za afya ya msingi na Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuongeza upatikanaji wa huduma na kupunguza vifo vitokanavyo na ugonjwa huo.

Kuhusu ufadhili, Rais Samia alisema Serikali kupitia Mabaraza ya Kutokomeza Malaria Tanzania Bara na Zanzibar inaendelea kushirikiana na sekta binafsi, taasisi za dini, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo kuhamasisha rasilimali za ndani.
Pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa akitaja taasisi kama Global Fund na Benki ya Dunia kuendelea kutekeleza ahadi zao katika kufadhili programu za malaria barani Afrika.

Kwa upande wake, Rais wa Botswana na Mwenyekiti wa ALMA, Mheshimiwa Duma Gideon Boko, akitoa takwimu za Ripoti ya Maendeleo ya Malaria Afrika 2025, alisema bara hilo bado liko mbali kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030, akihimiza nchi wanachama kutenga bajeti mahsusi na kuimarisha mifumo ya takwimu.

Naye Kamishna wa Afya, Masuala ya Binadamu na Maendeleo ya Jamii wa Umoja wa Afrika, Balozi Amma Twum-Amoah, alisema kupungua kwa ufadhili wa kimataifa kumeathiri juhudi za mapambano dhidi ya malaria na kusisitiza haja ya mifumo imara ya afya, ushiriki wa sekta binafsi na mikakati inayozingatia athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, mkutano huo umewaleta pamoja Wakuu wa Nchi, Mawaziri wa Afya na wadau wa maendeleo kujadili Ripoti ya Maendeleo ya Malaria Afrika 2025, inayoonyesha kuwa Afrika inabeba zaidi ya asilimia 90 ya maambukizi na vifo vya malaria duniani, huku msukumo mpya ukihitajika kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.  

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254




Post a Comment

Previous Post Next Post