" SERIKALI YAONDOA MASHARTI MAGUMU YA MIKOPO, YATENGA SH BILIONI 200 KUWAWEZESHA VIJANA KIUCHUMI

SERIKALI YAONDOA MASHARTI MAGUMU YA MIKOPO, YATENGA SH BILIONI 200 KUWAWEZESHA VIJANA KIUCHUMI

 

Na Mapuli Kitina Misalaba

Serikali imesema imeondoa masharti magumu yaliyokuwa kikwazo kwa vijana kunufaika na mikopo, ikiwamo dhamana isiyohamishika, ili kupanua wigo wa upatikanaji wa fedha za uwezeshaji kiasi cha Shilingi bilioni 200 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka, wakati wa uzinduzi wa Jukwaa la Vijana Mkoa wa Shinyanga uliofanyika Ukumbi wa Lyakale, Manispaa ya Shinyanga, ambapo alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata mitaji bila vikwazo visivyo vya lazima.

Amesema fedha hizo zimetengwa mahsusi kwa vijana na zimesambazwa katika sekta mbalimbali zikiwamo Wizara za Mifugo na Uvuvi, Kilimo, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, dhamira ya Rais ni kuona vijana wanakuwa wabunifu, wachapakazi na wenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi. Ametolea mfano Mkoa wa Mwanza ambako vijana tayari wamenufaika na Sh milioni 200 kupitia mpango huo.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali iko mbioni kuanzisha dawati maalumu la vijana ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) litakaloshughulikia masuala ya kodi kwa vijana, hatua inayolenga kuweka mazingira rafiki ya ulipaji kodi na uendeshaji wa biashara zao.

Katika kusisitiza dhamira hiyo, Waziri Nanauka amesema Serikali pia imeendelea kuwekeza katika kuwajengea vijana ujuzi kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ambapo Sh bilioni 3 zimetolewa na vijana wengi tayari wananufaika na mafunzo ya ufundi stadi.

Amewataka vijana kuwa na ndoto, nidhamu ya muda na kujituma, akibainisha kuwa vijana ni nguvu kazi muhimu inayochangia takribani asilimia 55 ya uzalishaji nchini.

Uzinduzi wa Jukwaa la Vijana Mkoa wa Shinyanga umeelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha mawasiliano ya moja kwa moja na vijana, kuwafikishia taarifa sahihi za fursa na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka akizungumza kwenye uzinduzi wa Jukwaa la Vijana Mkoa wa Shinyanga leo Jumamosi Febuari 21, 2026.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Mhe. Joel Nanauka akizungumza kwenye uzinduzi wa Jukwaa la Vijana Mkoa wa Shinyanga leo Jumamosi Febuari 21, 2026.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Dkt. Kedmon Mapana akizungumza kwenye uzinduzi wa Jukwaa la Vijana Mkoa wa Shinyanga leo Jumamosi Febuari 21, 2026.



 

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post