" SIMBA YAKABIDHIWA MILIONI 5 ZA GOLI LA MAMA

SIMBA YAKABIDHIWA MILIONI 5 ZA GOLI LA MAMA





Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Msigwa akikabidhi fedha za GOLI LA MAMA leo Februari 21, 2026, Morena Hotel, Dodoma, kwa timu ya Simba Sports Club kufuatia ushindi wao wa bao 1 -0 dhidi ya Stade Malien katika mashindano ya Club Bingwa Afrika uliochezwa Februari 14, 2026, katika Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.

Na. Mwandishi Wetu – MAELEZO

Klabu ya Simba imepokea zawadi ya shilingi milioni Tano (5,000,000/=) kama “Goli la Mama” kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kufuatia ushindi wao muhimu wa bao 1-0 dhidi ya Stade de Malien ya Mali, katika mechi iliyochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Februari 14, 2026.

Zawadi hiyo imekabidhiwa leo Februari 21, 2026 jijini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, kama pongezi kwa ushindi huo uliopatikana katika hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akikabidhi fedha hizo, Msigwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kutambua mchango wa michezo katika kuimarisha umoja wa kitaifa na kulitangaza taifa kimataifa, huku akizitaka klabu nyingine kuiga mfano na juhudi za Simba za kupambana kwa bidii katika mashindano ya kimataifa.

‘Mhe. Rais anawashukuru na kuwapongeza sana kwa ushiriki wenu katika Mashindano haya ya kimataifa na anaamini kuwa matokeo ya ushiriki wa simba katika mashindano haya yatakuwa yametuachia somo na tutakwenda kujipanga vizuri ili tuweze kufanya vizuri zaidi katika mashindano yajayo. Mhe. Rais anaamini Simba ni timu nzuri pia ina mipango mizuri na uongozi mzuri ambao unaweza kutufikisha katika malengo ya kimataifa” amesema Msigwa.



Msigwa amesema katika mchezo huo Simba ilionesha kiwango cha juu na kufanikiwa kuondoka na alama tatu muhimu katika kinyang’anyiro hicho cha klabu bingwa barani Afrika.

Ushindi huo unaongeza matumaini kwa mashabiki wa Simba na kuimarisha nafasi ya timu hiyo katika kundi lake, huku “Goli la Mama” likiendelea kuwa chachu ya hamasa kwa vilabu vinavyopeperusha bendera ya Tanzania katika anga za kimataifa.

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment

Previous Post Next Post