
Na WMJJWM – Dodoma
Serikali imetoa mwongozo rasmi wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwa mwaka 2026, yatakayofanyika kuanzia Machi 1 hadi 8 kote nchini.
Hayo yamebainishwa Februari 17, 2026 na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, wakati akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma, ambapo amesema maadhimisho hayo yatafanyika kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa yakiongozwa na mwongozo maalum uliotolewa na Wizara.
Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka 2026 ni “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050”, ikilenga kujenga uelewa wa kuwekeza katika maendeleo jumuishi kwa kutambua na kutekeleza haki za wanawake na wasichana kwa vitendo.
Amesisitiza kuwa kaulimbiu hiyo imejikita katika nguzo za Dira ya Taifa ya 2050 na inahusisha makundi yote ya kijamii.
Katika mwongozo huo, Waziri Dkt. Gwajima ameeleza kuwa kila mkoa utawajibika kuratibu maadhimisho na kutoa taarifa kwa umma kuhusu ratiba na maudhui ya shughuli zitakazofanyika. Aidha, sare rasmi ya maadhimisho itakuwa vazi la batiki, ambapo kila mkoa utahamasishwa kutumia wazalishaji wa ndani ili kuinua uchumi wa wajasiriamali wa ndani, hususan wanawake.
Amefafanua kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanajengwa juu ya misingi ya Ulingo wa Beijing wa mwaka 1995 unaolenga kukuza usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kupitia ajenda 12 muhimu, ikiwemo kupinga umaskini, ukatili wa kijinsia, kuboresha afya na elimu, pamoja na kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi na uchumi.
Aidha, amesema maadhimisho hayo yatahusisha midahalo, makongamano, maonesho ya wajasiriamali, uzinduzi wa miradi ya kijamii, mashindano ya kielimu na michezo ya kuelimisha, utoaji wa tuzo kwa wanawake vinara pamoja na matembezi ya hiari siku ya kilele. Pia, wananchi wataelimishwa kuhusu huduma za msaada wa kisheria, uwezeshaji wa kiuchumi na maadili ya jamii.
Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa maadhimisho hayo hayahusiani na itikadi yoyote bali ni ya wanawake wote kwa kushirikiana na wanaume kama wadau wakuu wa maendeleo. Amevitaka vyombo vya habari kutoa ushirikiano ili kuhakikisha taarifa za maadhimisho zinawafikia wananchi wote, huku akibainisha kuwa Wizara itaungana na Mkoa wa Geita katika maadhimisho hayo na tathmini ya ushiriki wa mikoa itatolewa Machi 30, 2026.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment