Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, amebainisha kuwa mafanikio ya mipango ya Serikali katika kutatua changamoto ya ajira nchini yanategemea kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa amani na utulivu wa kudumu.
Amesema kuwa mazingira tulivu ndiyo kivutio kikuu kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, ambao wana nafasi kubwa ya kuanzisha miradi itakayozalisha nafasi nyingi za kazi kwa Watanzania.
Aidha Waziri Sangu, ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha mahusiano mema miongoni mwao ili kuimarisha umoja wa Taifa na kuchochea kasi ya maendeleo endelevu nchini.
Waziri Sangu ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao cha wadau wa mahusiano kilichofanyika Februari 24, 2026, katika Halmashauri ya Sumbawanga mkoani Rukwa.
Katika hotuba yake, Waziri Sangu amebainisha kuwa Serikali imejipanga kuendelea kuratibu na kuimarisha mahusiano kati yake na makundi mbalimbali ya kijamii. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa Tanzania inaendelea kusalia kuwa kielelezo cha amani na utulivu barani Afrika, sifa ambayo imekuwa ikilitofautisha Taifa hili kwa miongo mingi.
Aidha, Waziri huyo amefafanua kuwa sifa kuu inayomtambulisha Mtanzania duniani kote ni mahusiano mazuri yanayojengwa katika misingi mikuu mitatu. Msingi wa kwanza ni mila na desturi za nchi ambazo zimejenga historia ndefu ya ushirikiano na utani miongoni mwa makabila mbalimbali, jambo linalopunguza mivutano na kuleta ukaribu.
Vilevile, amesisitiza kuwa msingi wa pili unategemea mifumo imara ya kisera, kisheria na miongozo mbalimbali inayosimamia mahusiano nchini. Msingi wa tatu na wa mwisho ni umoja na mshikamano wa dhati ambao uliachwa na kurithishwa na waasisi wa Taifa hili, ambao unapaswa kulindwa kwa nguvu zote ili kuendeleza tunu hiyo kwa vizazi vijavyo.
Waziri Sangu amefafanua kuwa bila kuwepo kwa mahusiano mema na utulivu wa kijamii, ni vigumu kwa wawekezaji kuweka mitaji yao nchini, jambo ambalo linaweza kukwamisha jitihada za Serikali za kukuza uchumi. Hivyo, amesisitiza kuwa jukumu la kulinda amani si la vyombo vya dola pekee, bali ni la kila mwananchi ili kutengeneza mazingira rafiki yanayochochea ukuaji wa sekta za uzalishaji na huduma.
Aidha, ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya kisheria na kisera ili kuhakikisha kuwa uwekezaji unaoingia nchini unatoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa. Amesema kuwa kupitia utulivu uliopo, wananchi wataweza kunufaika na fursa mbalimbali zitakazojitokeza, huku kukiwa na msisitizo wa kudumisha nidhamu na tija mahali pa kazi ili kuvutia uwekezaji zaidi.
Waziri Sangu ametoa wito kwa wadau wa mahusiano na kazi nchini kuona umuhimu wa majadiliano na maridhiano kama njia bora ya kutatua migogoro. Amesema kuwa mahusiano imara mahali pa kazi yanachangia kuwepo kwa mazingira bora ya biashara, ambayo hatimaye yanatengeneza mnyororo wa thamani unaozalisha ajira endelevu na kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment