Na Fabius Clavery Misalaba Media-Kagera.
Hali ya michezo wilayani Biharamulo imepanda chati baada ya Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, Mhe. Eng. Ezra John Chiwelesa, kushirikiana na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera, Mhe. Samira Khalfan Amour, kuwaunga mkono wanafunzi na wadau wa michezo kuelekea mashindano ya UMISSETA Mwaka 2026.
Februari 21, 2026, Eng. Chiwelesa ameongoza zoezi la kugawa seti za jezi na mipira kwa shule zote (35) za sekondari za serikali na binafsi wilayani humo ,huku Mhe. Samira akichangia kilo 500 za mchele kwa ajili ya lishe ya wanafunzi watakaoshiriki mashindano hayo.
Zoezi hilo la ugawaji wa vifaa limefanyika katika Uwanja Wa Shule ya sekondari Kagango wavulana,Hatua hiyo imeongeza hamasa na morali kwa vijana wanaojiandaa kupeperusha bendera ya Biharamulo, mashindano hayo yanayotarajiwa kuanza kurindima hivi karibuni.
Akizungumza katika hafla hiyo, Eng. Chiwelesa amesisitiza kuwa maandalizi ya mapema ni silaha ya ushindi, akiwataka walimu na viongozi wa shule kusimamia vyema matumizi ya vifaa hivyo ili viweze kuleta tija iliyokusudiwa.
Aidha Mbunge huyo Ameahidi kutoa Kiasi cha Tshs 5,000,000/= (Milioni tano) kwaajili ya Kambi ya UMISSETA 2026 ili Kusaidia mahitaji mbalimbali wakati Kambi hiyo ngazi ya wilaya.Aidha amehaidi kuendelea kutoa shilingi milioni Tano kila mwaka kwa ajili ya Timu ya wilaya katika mashindano hayo ya UMISSETA kwa timu ya Wilaya ya Biharamulo.
Kwa upande wake, Mhe. Samira Khalfan ameeleza kuwa uwekezaji katika michezo si tu hujenga afya na nidhamu, bali pia huibua vipaji na kufungua milango ya mafanikio kwa vijana katika taifa hili.
Mhe.Samira ametoa wito kwa wazazi kuwekeza kwenye vipaji vya watoto kwani nisehemu ya fursa za ajira kote duniani kwa sasa.Juhudi hizo zinaenda sambamba na maono ya Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha michezo shuleni kama chachu ya maendeleo ya vijana kiafya, kinidhamu na kitaaluma.
Zoezi hilo limepokelewa kwa furaha na wanafunzi, walimu na wadau wa michezo, wengi wakiamini kuwa msaada huo ni kichocheo muhimu kuelekea mafanikio makubwa ya Biharamulo kwenye UMISSETA 2026.




Post a Comment