" WANNE MBARONI KWA KUSAFIRISHA BANGI, NDUGU WATATU WASHIKILIWA KWA MAUAJI MBEYA

WANNE MBARONI KWA KUSAFIRISHA BANGI, NDUGU WATATU WASHIKILIWA KWA MAUAJI MBEYA






Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wanne kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 45 na gramu 785 katika nyakati tofauti.

Watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Wilfred Komba (24), mwanafunzi wa mwaka wa kwanza Chuo Kikuu cha Iringa, Lenad Shamba maarufu Paulo (21) mkazi wa Tarime mkoani Mara, James Mwakalebela (26) mkazi wa Ngonga – Kyela na Joseph Mkwara maarufu Aliki (26) mkazi wa Kyela.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa wanasafirisha dawa hizo zikiwa zimehifadhiwa katika mabegi matatu na mifuko miwili ya sandarusi wakitumia mabasi ya abiria kutoka Mbeya kuelekea Dar es Salaam. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa dawa hizo ziliingizwa nchini kutoka nchi jirani.

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi linawashikilia ndugu wa familia moja ambao ni Solomon Mwambyale (68) pamoja na watoto wake wawili, Stephano Mwaisango (32) na Emmanuel Mwaisango (36), wote wakazi wa Busoka – Masebe, kwa tuhuma za kumuua Jenti Segelela (87) ambaye ni shemeji wa Solomon Mwambyale.

Tukio hilo lilitokea Februari 7, 2026 katika Kitongoji cha Busoka, Kijiji cha Lusungo, Kata ya Makwale ambapo inadaiwa kuwa mtuhumiwa kwa kushirikiana na watoto wake walimuua marehemu kwa kumkata na kitu chenye ncha kali sehemu ya shingo kisha kutoroka.

Kufuatia tukio hilo, askari wa Jeshi la Polisi kitengo cha uchunguzi wa mauaji walianzisha msako mkali na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wote watatu Februari 8, 2026 majira ya saa 1:00 usiku. Uchunguzi wa awali umeonesha chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa mashamba ya ukoo na tamaa ya kujipatia mali kwa njia isiyo halali.

Aidha, Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wawili, Charles Oden maarufu Mwakasege (32), fundi simu mkazi wa Meta, na Isack Charles maarufu Bebwa, mkazi wa Shewa Jijini Mbeya, kwa tuhuma za kuingilia mifumo ya kibiashara ya makampuni ya ukopeshaji simu.

Watuhumiwa hao walikamatwa katika misako iliyofanyika kati ya Januari 27 na Februari 5, 2026 katika eneo la Mtaa wa Rungwe Music, Mwanjelwa Jijini Mbeya. Inadaiwa walikuwa wakibadili na kuondoa mifumo maalum iliyowekwa kwenye simu zilizokopwa ili kuwafanya waliokopeshwa washindwe kufuatiliwa kulipa madeni yao.

Baada ya upekuzi katika ofisi zao, polisi walikuta simu mbalimbali zikiwemo Samsung A53, Infinix 21, Tecno 13, Itel 11 na YAS 1 pamoja na vifaa vya kuflashia simu kama Infinity Box Dongle CM2, JTAG Adapter ISP 4bit, F64 Flash Ultra Box, Easy JTAG Plus Box, UFI Box na Laptop tatu.

Ukaguzi wa awali umebaini baadhi ya simu hizo zinamilikiwa na makampuni ya ukopeshaji huku nyingine zikitambuliwa kuwa ni mali zilizoibiwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limetoa wito kwa wananchi kuacha kujihusisha na uingizaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya, likisisitiza kuwa ni kinyume cha sheria na ni hatari kwa afya, hususan kwa vijana. Aidha, limetoa rai kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kwa lengo la kujipatia mali kuacha mara moja na kujihusisha na shughuli halali, likisisitiza kuwa uhalifu haulipi na hauna nafasi katika jamii.

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment

Previous Post Next Post