" YOGE YAPELEKA TABASAMU KWA WANANCHI WA MBINGA KUPITIA MRADI WA SAUTI ZA MAJI

YOGE YAPELEKA TABASAMU KWA WANANCHI WA MBINGA KUPITIA MRADI WA SAUTI ZA MAJI

Na Mwandishi wetu, Misalaba MediaWilaya ya Mbinga imepata tumaini jipya la upatikanaji na uhifadhi wa maji kufuatia uzinduzi wa Mradi wa utunzaji wa mazingira unaojulikana kama ‘Sauti za Maji’. Mradi huo umezinduliwa rasmi  na Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Bi. Pendo Daniel, katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, ukihusisha Halmashauri ya Mji Mbinga pamoja na wadau wa maji na mazingira.Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Bi. Pendo Daniel alimpongeza Wakili Philomena Mwalongo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Youth Environmental Justice and Gender Equality (YOGE), kwa kuleta mradi huo wenye tija katika bonde la Ruvuma River Basin. Ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia utawala shirikishi unaolenga usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu kwa jamii zinazoishi kandokando ya bonde hilo.Aidha, Kaimu Mkuu huyo wa Wilaya ameonesha matumaini makubwa kuwa mradi huo utaleta manufaa kwa wananchi kupitia utoaji wa elimu ya nishati mbadala na mbinu bora za utunzaji wa mazingira. Amesisitiza kuwa kulinda vyanzo vya maji ni jukumu la kila mwananchi, na kwamba ushirikishwaji wa makundi yote ya kijamii ni msingi wa mafanikio ya mpango huo.Kwa upande wake, Wakili Philomena Mwalongo aliishukuru Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbinga kwa mapokezi mazuri na ushirikiano wanaoupata. Ameeleza kuwa lengo kuu la mradi wa ‘Sauti za Maji’ ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu uhifadhi wa rasilimali za maji na mazingira, huku ukitoa kipaumbele kwa wanawake, vijana na makundi maalum ili kuimarisha usawa wa kijinsia katika maendeleo.Mradi huo unatarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi Machi 2026 katika Halmashauri ya Mji Mbinga, ukilenga wananchi wanaoishi katika bonde la Mto Ruvuma. Kupitia ushirikiano kati ya YOGE na Tanzania Media for Community Development (TAMCODE), jamii inatarajiwa kunufaika na elimu, uhamasishaji na hatua madhubuti za kulinda mazingira na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali za maji kwa kizazi cha sasa na kijacho.

  

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



 

Post a Comment

Previous Post Next Post