" ASKOFU MSTAAFU WA JIMBO KUU KATOLIKI IRINGA TARCISIUS NGALALEKUMTWA AWAFARIJI WAUMINI: “KIFO SI LAANA, NI WITO WA MUNGU”

ASKOFU MSTAAFU WA JIMBO KUU KATOLIKI IRINGA TARCISIUS NGALALEKUMTWA AWAFARIJI WAUMINI: “KIFO SI LAANA, NI WITO WA MUNGU”






NA DENIS MLOWE, IRINGA

ASKOFU mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Iringa, Tarcisius Ngalalekumtwa, ametoa ujumbe wa faraja kwa waumini akihubiri kuwa kifo cha mwanadamu si laana wala maangamizi, bali ni wito kutoka kwa Mungu na njia ya kuelekea uzima wa milele.

Akizungumza katika ibada inaliyofanyika leo katika Kanisa Kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu lililopo Kihesa, Askofu Ngalalekumtwa alisema uhai wa mwanadamu haupotei, bali unamezwa na kuingizwa katika utukufu, heri na baraka za milele.

Alisisitiza kuwa kifo hakipaswi kutazamwa kama adhabu, bali ni kurudi nyumbani kwa Muumba.

“Tusihuzunike kupita kiasi, kwani kifo ni mlango wa kuingia katika uzima wa milele,” alisema.

Aidha, aliwakumbusha waumini kuwa Yesu Kristo ndiye njia ya kweli na uzima, na kwamba wanaomwamini hupata tumaini la uzima wa milele.

Katika mahubiri hayo, Askofu Ngalalekumtwa alimtaja marehemu William Lukuvi akieleza kuwa alimtazama Kristo kwa upendo na amani, na sasa amehamia makao ya watakatifu alikoitwa na Mungu.

Awali Wakili Sosten Mbedule alisema maisha ya marehemu Lukuvi ni kielelezo cha uvumilivu, uadilifu, uzalendo na upendo kwa wananchi na taifa. Alisema marehemu alianza utumishi wake katika ngazi za chini na kupanda hatua kwa hatua hadi kuwa kiongozi wa taifa, jambo linalotoa funzo la kutokata tamaa.

Mbedule aliongeza kuwa marehemu alikuwa mpenda haki na mzalendo aliyeaminiwa katika majukumu mbalimbali ya kitaifa na aliyejitolea kutumika kokote alikohitajika. “Nilifanya naye kazi kwa karibu, na unaweza kuona alikuwa mtu wa haki na aliyesimama katika kutenda mema,” alisema.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (MNEC), Richard Kasesela, alieleza kuwa kifo cha Lukuvi ni pigo kubwa kwa mkoa wa Iringa, akimtaja kama mlezi, mwalimu na kiongozi aliyekuwa na ushawishi mkubwa. Alisema marehemu ndiye aliyemshawishi kuingia katika Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kipindi akiwa mwanafunzi wa Azania Secondary School.

Kasesela aliongeza kuwa katika uongozi wake, marehemu Lukuvi alikuwa mshauri muhimu hasa wakati wa majukumu yake kama mkuu wa wilaya. Alimtaja marehemu kama mtu aliyependa amani na aliyekuwa hana makundi ya kisiasa baada ya uchaguzi, bali alijiunga moja kwa moja kufanya kazi na aliyeshinda.

Akizungumzia kazi za marehemu katika jimbo lake, Kasesela alisema Lukuvi alikuwa mstari wa mbele kusaidia wananchi hasa katika majanga kama mafuriko ya Pawaga, ambapo mara nyingi alikuwa wa kwanza kufika na kusaidia waathiriwa.

Alimalizia kwa kusema kuwa marehemu alikuwa mtumishi wa watu, aliyekuwa akitumia mishahara yake kusaidia jamii na kushughulikia kero za wananchi.

Waumini waliendelea kuomboleza kwa unyenyekevu wakimuomba Mungu ampokee marehemu katika pumziko la milele.
 
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post