Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), yatakiwa kuongeza kasi ya urasimishaji wa biashara na kuimarisha mifumo ya kidijitali ili kuchochea ufanisi na ukuaji wa uchumi kwani BRELA ni lango kuu la uwekezaji nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb), Machi 04, 2026, wakati akifungua Baraza la wafanyakazi la BRELA na kuhimiza uwekezaji kwenye rasilimali watu, akitaka watumishi wapewe mafunzo na stahiki zao kwani ustawi wa wafanyakazi ndio siri ya mafanikio ya taasisi, na kuwataka watumishi kufanya kazi kwa uadilifu, weledi, na uzalendo.
Waziri Kapinga amebainisha kuwa kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za wadau, zaidi ya 80% ya biashara nchini zipo sekta isiyo rasmi, hivyo BRELA lazima iwe kinara wa kuzirasimisha, hatua ambayo itawawezesha Wajasiriamali wadogo kupata mikopo, masoko, na ulinzi wa kisheria.
Aidha, ameagiza kuhuisha mifumo ya TEHAMA ili iwe rafiki itakayopunguza gharama pamoja na muda wa mteja kupata huduma na kusisitiza kuwa mifumo hiyo lazima iwe na usalama wa taarifa wa hali ya juu na itumike kupata mrejesho wa haraka kutoka kwa wateja ili kuboresha utendaji.
Aidha, ameipongeza BRELA kwa ongezeko la usajili na makusanyo, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyakazi na kuitaka taasisi hiyo kugeukia mfumo wa uwezeshaji badala ya udhibiti pekee ili kukuza sekta binafsi nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa BRELA Bw. Godfrey Nyaisa amebainisha kuwa BRELA imevuka lengo la mapato kwa asilimia 105 na kutekeleza malengo kwa asilimia 78 katika nusu mwaka wa 2025/26, ambapo taasisi hiyo imewasilisha Shilingi bilioni 3.1 kwa Msajili wa Hazina, na kusema mafanikio hayo yanayotokana na mshikamano, kujituma na bidii ya watumishi.
Vilevile, amewasilisha Mpango Mkakati wa 2026–2031 unaolenga kuboresha za usajili na miundombinu, ikiwemo ujenzi wa ofisi za Dodoma na Kinondoni na kubainisha kuwa uongozi unaendelea kuimarisha maslahi ya watumishi kupitia muundo mpya wa mishahara na motisha ili kutatua changamoto za uhaba wa wafanyakazi na kuongeza tija.



🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment