" MBUNGE WA MPANDA MJINI AKUTANA NA MAKUNDI MAALUM NA MAFUNDI VIATU

MBUNGE WA MPANDA MJINI AKUTANA NA MAKUNDI MAALUM NA MAFUNDI VIATU


Na Mapuli Kitina Misalaba

Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, Mhe. Haidary Hemed Sumry, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Wazazi Taifa kutoka Mkoa wa Katavi, leo Machi 5, 2025 amekutana na makundi maalum pamoja na mafundi viatu katika jimbo hilo kwa lengo la kujitambulisha na kufahamiana na wananchi wake.

Katika hafla hiyo, Mhe. Sumry ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wananchi kwa kumpigia kura za ndiyo katika uchaguzi uliopita na kumchagua kuwa mwakilishi wao bungeni, akiahidi kuendelea kushirikiana nao katika kuwaletea maendeleo.

Aidha, amewasisitiza wananchi hao kuendelea kudumisha umoja, mshikamano na ushirikiano ili kuimarisha maendeleo katika jamii yao.

Pia amewahimiza mafundi viatu na makundi mengine kuunda vikundi rasmi vitakavyowawezesha kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali, ikiwemo mikopo ya riba nafuu kwa ajili ya kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Mhe. Sumry amesema serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wananchi kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli ndogo na za kati, hivyo ni muhimu kwa makundi hayo kujiandaa na kutumia fursa hizo ipasavyo ili kuboresha maisha yao.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi na mafundi viatu waliohudhuria mkutano huo wamemshukuru mbunge huyo kwa kuwatembelea na kuwasikiliza, wakiahidi kushirikiana naye katika kuendeleza juhudi za maendeleo katika Jimbo la Mpanda Mjini.

Akizungumza kwa niaba ya Chama, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Ndugu Jimotoli Jilala Maduka, amewahimiza wananchi kuendelea kumuunga mkono Mbunge wao katika juhudi za kuleta maendeleo jimboni humo.

Amesema ushirikiano kati ya wananchi na viongozi wao ni muhimu katika kuhakikisha mipango ya maendeleo inatekelezwa kwa ufanisi, huku akiwataka wananchi kudumisha umoja, mshikamano na kuendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.

Aidha, ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuimarisha maendeleo ya wananchi kupitia miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi nchini.

Katika hafla hiyo pia, Kaimu Mkurugenzi wa SIDO Mkoa wa Katavi, Ndugu Baraka Kaimu, ametoa elimu kwa wananchi kuhusu fursa za ujasiriamali na namna ya kunufaika na huduma zinazotolewa na Small Industries Development Organization, akiwahimiza wananchi kuunda vikundi na kutumia mafunzo pamoja na mikopo ya riba nafuu ili kukuza shughuli zao za kiuchumi na kujiongezea kipato.

 

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

 

Post a Comment

Previous Post Next Post