" MKAKATI WA MKUMBI II: FURSA MPYA KWA KIJANA MBUNIFU NA MUSTAKABALI WA UCHUMI WA TAIFA

MKAKATI WA MKUMBI II: FURSA MPYA KWA KIJANA MBUNIFU NA MUSTAKABALI WA UCHUMI WA TAIFA


Hatua ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kuandaa Mkakati wa Pili wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI II) ni habari njema sana kwa kijana wa Kitanzania anayewaza kujikwamua kiuchumi. 

Kupitia maeneo kumi na moja yaliyoainishwa na Profesa Kitila Mkumbo, serikali inakwenda kufanya mageuzi makubwa yatakayoondoa vikwazo hamsini na tisa vilivyokuwa vikiwakwamisha wajasiriamali wadogo na wakubwa. 

Kwa kijana, hii ina maana kuwa ule urasimu wa kuanzisha biashara, ugumu wa kupata mitaji, na changamoto za masoko sasa vinakwenda kupatiwa ufumbuzi kupitia hatua za kimageuzi zaidi ya mia mbili, jambo litakalofanya kuanzisha kampuni au mradi wa kibiashara kuwa rahisi na wenye tija zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Maana kubwa ya mkakati huu kwa taifa ni kuandaa mazingira ya kufikia azma ya kuwa na uchumi wa thamani ya dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050. Ili kufika huko, serikali inatambua kuwa maendeleo ya kweli yanaletwa na ubunifu, na ubunifu unastawi pale tu ambapo mazingira ya biashara yanaruhusu ushindani wa haki. 

Kwa kijana, "mazingira ya kidijiti" na "nguvukazi ya stadi" zilizotajwa kwenye mkakati huu ni fursa ya dhahabu. Serikali inatambua kuwa dunia ya sasa inategemea teknolojia, hivyo mkakati huu unakwenda kulinda hakimiliki za vijana wabunifu na kuwapa ujuzi unaoendana na soko la ajira la sasa, ili wasiishie kuwa na vyeti tu bali wawe na uwezo wa kuzalisha mali.

Eneo lingine muhimu ambalo vijana wanapaswa "kujishika" ni katika soko la ndani ya Afrika na Jumuiya za Kikanda kama SADC na Afrika Mashariki. Profesa Kitila amebainisha kuwa nchi za Afrika zinafanya biashara kati yao kwa asilimia kumi na sita tu, huku kiasi kikubwa cha biashara kikifanywa na mabara ya mbali.

 Hapa ndipo kijana wa Kitanzania anapaswa kuelekeza macho yake; badala ya kuwaza kuuza bidhaa au huduma ndani ya kijiji au mkoa wake pekee, anapaswa kutumia maboresho haya ya MKUMBI II kuwaza soko la Afrika. Hii ni fursa ya kutengeneza bidhaa zinazokidhi viwango vya kimataifa ili kunufaika na soko huru la Afrika ambalo lina mamilioni ya walaji.

Kijana anapaswa kujishika kwenye eneo la "kubadili mitazamo na uwajibikaji" kama ilivyoainishwa katika rasimu hiyo. Maendeleo hayaji kwa kulalamika au kusubiri ajira za serikali pekee, bali yanakuja kwa kijana kuchangamkia fursa za uwekezaji na kutoa maoni yake kwenye rasimu hii ambayo bado iko hadharani. 

Huu ni wakati wa vijana kusoma nyaraka hizi za serikali, kuelewa mwelekeo wa nchi, na kujiweka tayari kibiashara ili kuanzia mwezi Julai mkakati huu utakapoanza kutekelezwa rasmi, wawe tayari wamejipanga kuitumia miundombinu, mitaji, na masoko yatakayokuwa yameboreshwa.

MKUMBI II ni daraja linalounganisha ndoto za vijana na uhalisia wa kiuchumi wa nchi. Kijana mwenye stadi, mbunifu, na mzalendo hawezi kuachwa nyuma na mfumo huu mpya unaolenga kuondoa rushwa na urasimu. Jukumu la vijana sasa ni kuacha kuangalia vikwazo vya nyuma na kuanza kuangalia fursa za mbele, wakijua kuwa serikali imeweka mazingira rafiki ili wao waweze kuwa injini ya ukuaji wa uchumi kuelekea Dira ya mwaka elfu mbili hamsini. Huu ni wakati wa kazi, ubunifu, na ushindani wa tija kwa manufaa ya kizazi hiki na kijacho.

 

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment

Previous Post Next Post