Na Gabon Mariba, Mara.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Ndugu Crispin Chalamila amefanya ziara ya kikazi katika Mkoa wa Mara ambapo pamoja na mambo mengine amekabidhi vifaa tiba katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kufungua ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Bunda.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Ndugu Chalamila amesema TAKUKURU kwa sasa imejikita zaidi katika kuzuia rushwa kupitia utoaji wa elimu kwa wananchi, ukaguzi wa mifumo ya utendaji kazi pamoja na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Amesema taasisi hiyo pia inaendelea kushirikiana na jamii katika kuhakikisha vitendo vya rushwa vinadhibitiwa ili kulinda rasilimali na fedha za umma.
Katika hatua nyingine, Ndugu Chalamila alikabidhi mashine maalum za kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya muda katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, ambapo amesema msaada huo umetolewa baada ya utafiti kubaini kuwa hospitali nyingi zinakosa mashine hizo muhimu.
Ameeleza kuwa utoaji wa vifaa hivyo ni sehemu ya kurudisha kwa jamii, huku akibainisha kuwa Mkoa wa Mara ni mkoa wa 15 kupokea msaada huo katika hospitali za rufaa za mikoa.
Awali katika ziara hiyo, Ndugu Chalamila alifungua rasmi jengo la ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Bunda pamoja na kuzungumza na watumishi wa taasisi hiyo.
Katika ziara hiyo pia, Ndugu Chalamila alikutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Kanali Evans Alfred Mtambi ambaye alimkaribisha mkoani humo na kumpongeza kwa juhudi za taasisi hiyo katika kudhibiti vitendo vya rushwa na kulinda fedha za umma.
Mhe. Mtambi amesema ushirikiano wa TAKUKURU katika Mkoa wa Mara umeendelea kusaidia Serikali kudhibiti matumizi mabaya ya fedha katika miradi ya maendeleo pamoja na kuongeza uwazi katika ukusanyaji wa mapato, hususan katika vivuko vinavyosimamiwa na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA).
Mapokezi hayo pia yalihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara Ndugu Gerald Musabila Kusaya, maafisa kutoka TAKUKURU Makao Makuu pamoja na Sekretarieti ya Mkoa wa Mara.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254













Post a Comment