" MKUU WA MKOA WA IRINGA KHERI JAMES AFUNGUA KONGAMANO LA WADAU WA HABARI, AIPONGEZA MISA TAN KWA KUIMARISHA WELEDI WA VYOMBO VYA HABARI

MKUU WA MKOA WA IRINGA KHERI JAMES AFUNGUA KONGAMANO LA WADAU WA HABARI, AIPONGEZA MISA TAN KWA KUIMARISHA WELEDI WA VYOMBO VYA HABARI


Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amefungua rasmi kongamano la wadau wa habari lililoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara,Tawi la Tanzania (MISA TAN) mkoani humo, huku akiipongeza taasisi hiyo kwa kuendelea kusimamia weledi na maendeleo ya sekta ya habari nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, James amesema ameridhishwa na maono ya MISA Tanzania katika kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari pamoja na kukuza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya jamii.

Amesema Mkoa wa Iringa unaendelea kukua kiuchumi kutokana na shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kilimo, biashara, elimu na uwekezaji wa viwanda, huku akitaja mazao kama mahindi na maharage kuwa miongoni mwa mazao muhimu yanayochangia uchumi wa mkoa huo.

James ameeleza kuwa Iringa pia ina vivutio mbalimbali vya utalii kama Bwawa la Mtela, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha pamoja na maeneo ya kihistoria kama historia ya Mtemi Mbwao, ambavyo vinaifanya mkoa huo kuwa na fursa nyingi za kiuchumi.

Aidha amesema upatikanaji wa huduma muhimu kama umeme, maji na miundombinu ya barabara umeendelea kuboresha maisha ya wananchi na kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali.

Katika hotuba yake, Mkuu huyo wa Mkoa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo imechangia kuboresha huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko, amesema kongamano hilo linalenga kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari na wadau wa maendeleo pamoja na kuendeleza uandishi wa habari unaolenga kutoa suluhisho kwa changamoto za jamii.

Soko amesema MISA Tanzania itaendelea kulinda uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza na haki ya kupata taarifa, huku akiwahimiza waandishi wa habari kuendelea kuandika wenye suluhisho kwa kuzingatia weledi wao.

Aidha ameeleza kuwa taasisi hiyo ina mpango wa kuanzisha kituo cha ugawaji wa taarifa za maendeleo kwa jamii, ambacho kitatoa elimu na taarifa muhimu kwa wananchi, na kuiomba serikali ya mkoa kutoa eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa amekubali ombi hilo na kusema serikali ya mkoa iko tayari kushirikiana na MISA Tanzania kwa kutoa eneo la kujenga kituo hicho cha taarifa.

Katika hatua nyingine, Meneja wa NSSF Mkoa wa Iringa, Benedict Wela, amesema taasisi hiyo inaendelea kuwahamasisha Watanzania kujiunga na mfumo wa hifadhi ya jamii ili kuwasaidia kujikinga na umaskini na kuwa na usalama wa kipato baada ya kustaafu.

Kongamano hilo limewakutanisha waandishi wa habari, wahariri, viongozi wa serikali pamoja na wadau mbalimbali kwa lengo la kujadili mchango wa sekta ya habari katika maendeleo ya Mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla.

Katika kongamano hilo pia yamefanyika majadiliano kuhusu jukumu la wahariri, viongozi wa taasisi na serikali kwenye mipango ya kuchochea mipango ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Uchumi, biashara na sekta za uzalishaji.


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James akifungua kongamano hilo.

Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Edwin Soko akizungumza.






  

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post