" MWALUNENGE NA DKT. TULIA WAUNGANA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI IYELA NA MWAKIBETE

MWALUNENGE NA DKT. TULIA WAUNGANA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WANANCHI IYELA NA MWAKIBETE

Na Lydia Lugakila-Misalaba media 

Mbeya 

Wabunge wawili, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Patrick Mwalunenge, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Uyole ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, wamekutana kujadili na kutafuta suluhisho la changamoto ya barabara inayounganisha majimbo hayo mawili.

Lengo la mkutano huo ni kuondoa adha wanazokumbana nazo wananchi wanaotumia barabara hiyo katika shughuli zao za kila siku.

Akizungumza kwa undani, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson alimueleza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya na Mbunge wa Mbeya Mjini, Mheshimiwa Patrick Mwalunenge, umuhimu wa kushirikiana na Serikali ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha zege.

 Ujenzi huo unaofanywa na wadau kwa kushirikiana na wananchi unalenga kuunganisha majimbo ya Uyole na Mbeya Mjini.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kufunguliwa kwa haraka kwa barabara ya Pipeline ili kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi katika kata za Mwakibete na Iyela, ambazo zinaunganisha majimbo hayo mawili.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya na Mbunge wa Mbeya Mjini, Mheshimiwa Patrick Mwalunenge, ameahidi kuchangia shilingi milioni kumi ili kusaidia kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha zege.

Pia ameahidi kufanya mkutano na wananchi wa Iyela ili kuhamasisha ushiriki wao katika kuchangia maendeleo hayo, ambayo tayari yameanza kufanywa na wananchi wa Bombambili kutoka kata ya Mwakibete.

Mheshimiwa Mwalunenge alieleza kuwa hii ni mara yake ya kwanza kufika katika eneo hilo linalounganisha majimbo hayo mawili, na ameonesha kufurahishwa na namna ambavyo wadau na wananchi wameungana kuanzisha maendeleo kabla ya Serikali kufika rasmi kusaidia mradi huo.



 

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post