" RAIS SAMIA ATOA MAAGIZO KUHARAKISHA MRADI WA MATANKI YA MAFUTA

RAIS SAMIA ATOA MAAGIZO KUHARAKISHA MRADI WA MATANKI YA MAFUTA





Viongozi pamoja, wananchi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi Mradi wa ujenzi wa Matanki ya kupokea mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam katika eneo la Kigamboni Mnadani Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Machi, 2026.
Viongozi pamoja, wananchi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi Mradi wa ujenzi wa Matanki ya kupokea mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam katika eneo la Kigamboni Mnadani Jijini Dar es Salaam, tarehe 03 Machi, 2026.

……………

Na Sophia Kingimali

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo mahsusi kwa wizara na taasisi za Serikali kuhakikisha mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokelea na kuhifadhi mafuta katika eneo la Kigamboni unatekelezwa kwa viwango vya kimataifa na kukamilika kwa wakati.

Pia, ameiagiza Wizara ya Nishati kuimarisha miundombinu ya hifadhi ya mafuta na kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya kutosha kukabiliana na misukosuko ya bei katika soko la dunia, akitaja kupanda kwa bei ya mafuta duniani kuwa ni changamoto inayoonyesha umuhimu wa kuwa na miundombinu madhubuti ya nishati.

Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi la mradi huo wa kimkakati leo Machi 3, 2026, jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema uwekezaji huo ni hatua muhimu katika kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji kwa nchi za ukanda na kimataifa.

Aidha, amesisitiza kuwa jiografia ya Tanzania inatoa fursa ya kuhudumia nchi zisizo na bandari na kwamba Serikali imedhamiria kuitumia vyema fursa hiyo.

Amesema kuwa maboresho yanayoendelea katika sekta ya bandari, reli na barabara yameongeza uwezo wa bandari ya Dar es Salaam kupokea meli kubwa zaidi na kuongeza ushindani wake kimataifa, akibainisha kuwa hatua hizo zimechangia kuongezeka kwa mapato ya Serikali na kuimarisha uchumi wa taifa.

Akizungumzia ushirikishwaji wa sekta binafsi, Rais Samia amesema uamuzi huo ulikuwa wa kimkakati na umeleta tija kubwa katika kuongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji wa bandari, huku akieleza kuwa fedha zilizookolewa zimeelekezwa katika miradi mingine ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa matanki hayo ya mafuta.

Katika maelekezo yake, Rais Dkt. Samia ameitaka Wizara ya Uchukuzi pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa kuzingatia ubora, usalama wa mazingira na muda uliopangwa.

“Mradi huu umetumia fedha nyingi za Watanzania, hivyo lazima ujengwe kwa viwango vinavyokubalika kimataifa,” amesisitiza Dkt. Samia.

Rais pia ametaka ushirikiano wa karibu kati ya wizara husika na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuimarisha mifumo ya uhakiki na ufuatiliaji wa shehena za mafuta kuanzia zinapowasili bandarini hadi zinaposambazwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuziba mianya ya upotevu wa mapato kwa kutumia mifumo ya kisasa na yenye uwazi.

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, amemshukuru Rais kwa kuendelea kutoa kipaumbele kwa sekta ya uchukuzi na kuahidi kuwa wizara yake itasimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo.

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uwezo wa bandari ya Dar es Salaam kuhudumia mafuta na kuimarisha usalama wa nishati nchini.

Rais Samia amehitimisha kwa kuwataka wakandarasi na washauri wa mradi kuhakikisha wanatekeleza kazi kwa uadilifu, ubora na kwa wakati ili kuwezesha mradi huo kuanza kufanya kazi mapema mwaka ujao, akieleza matumaini yake kuwa mradi huo utachangia kwa kiasi kikubwa kukuza biashara, ajira na mapato ya taifa.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Bw. Mbassa, amesema dhumuni kuu la mradi huo wa ujenzi ni kuongeza uwezo wa nchi kupokea na kuhudumia shehena za mafuta kwa ufanisi zaidi.

Amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha miundombinu ya bandari ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya soko la ndani na nchi jirani, sambamba na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya mafuta katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment

Previous Post Next Post