" SHIRIKA LA KIVULINI LAIMARISHA USHIRIKI WA WABABA KATIKA AFYA YA MAMA NA MTOTO KUPITIA MRADI WA GROW ENRICH KISHAPU

SHIRIKA LA KIVULINI LAIMARISHA USHIRIKI WA WABABA KATIKA AFYA YA MAMA NA MTOTO KUPITIA MRADI WA GROW ENRICH KISHAPU


Shirika la Kivulini kwa kushirikiana na shirika la World Vision linaendelea kutekeleza mradi wa Grow ENRICH unaolenga kuboresha afya ya mama na mtoto pamoja na kuhamasisha ushiriki wa wanaume katika masuala ya afya ya familia.

Moja ya shughuli za mradi huo imefanyika katika Kata ya Shagihilu, Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, ambapo wananchi walikutana katika mdahalo maalum uliolenga kujadili sababu za ushiriki mdogo wa wanaume katika masuala ya afya ya mama na mtoto pamoja na kutafuta suluhisho la changamoto hiyo.

Akizungumza katika mdahalo huo, Meneja wa Mradi kutoka shirika la Kivulini Mageni Malulu alisema kuwa mradi wa Grow ENRICH unafanya kazi katika nyanja mbalimbali kuhakikisha vifo vya mama na mtoto vinapungua katika jamii.

Alieleza kuwa mradi huo unafanya kazi kwa karibu na vituo vya afya na zahanati kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya ili kuboresha utoaji wa huduma bora kwa wananchi. Aidha, mradi huo pia unafanya kazi na wahudumu wa afya ngazi ya jamii pamoja na kuboresha baadhi ya miundombinu ya vituo vya afya.

Mageni Malulu aliongeza kuwa mradi huo pia umeanzisha vikundi mbalimbali ndani ya jamii ikiwemo vikundi vya “Baba Bora” ambavyo vinahusisha wanaume wanaotoa elimu na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kwa kuhamasisha ushiriki wa wanaume katika afya ya familia.

“Tunafahamu katika jamii nyingi baba ndiye mtoa maamuzi makubwa katika familia, hivyo tunatumia vikundi vya Baba Bora kuwafikia wanaume wengine na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika masuala ya afya ya mama na mtoto,” alisema.

Mbali na vikundi vya Baba Bora, mradi pia unashirikisha vikundi vya wanawake na mabinti viongozi pamoja na kundi la Sauti ya Umma na Utekelezaji lenye wajumbe 10 kutoka kila kijiji ambao hufuatilia masuala mbalimbali katika sekta za afya, kilimo na maendeleo ya jamii.

Katika mdahalo huo pia walishiriki makundi ya waendesha pikipiki (bodaboda) ambao wamepewa vizibao vyenye ujumbe wa elimu ya afya ili kusaidia kusambaza ujumbe huo kwa wananchi wengi zaidi wanaokutana nao katika shughuli zao za kila siku.

Mdahalo huo ulisimamiwa na Afisa Maendeleo wa Wilaya ya Kishapu Lailat Naimu Ramadhani, ambaye aliwaongoza wananchi kutoa maoni yao kuhusu sababu zinazochangia ushiriki mdogo wa wanaume katika masuala ya afya.

Baadhi ya sababu zilizotajwa na wananchi ni pamoja na tofauti kubwa ya umri kati ya baadhi ya wanandoa inayosababisha aibu kwa wanaume kuongozana na wake zao kliniki, hofu ya wanaume kupima afya zao hospitalini, pamoja na mila na desturi ambazo wakati mwingine zinachangia wanaume kuona kuwa kuwasindikiza wake zao hospitali ni jambo lisilofaa.

Wananchi pia walieleza kuwa baadhi ya wanaume wanaathiriwa na mitazamo ya zamani kuwa wanawake walijifungulia nyumbani bila kwenda kliniki, hivyo wengine huona si lazima kushiriki katika huduma za afya.

Aidha, wengine walieleza kuwa kwa muda mrefu elimu nyingi za afya zililenga zaidi mama na mtoto huku baba akionekana kusahaulika, hali ambayo ilichangia kupunguza ushiriki wake katika masuala ya afya ya familia.

Akizungumza katika mdahalo huo, Afisa Lishe wa Wilaya ya Kishapu Amrani Hemedi Iddi aliwasisitiza wanaume kushiriki kikamilifu katika kipindi chote cha ujauzito wa wake zao.

Alisema mara tu mwanamke anapogundulika kuwa mjamzito ni muhimu baba aanze kutoa ushirikiano wa karibu ikiwa ni pamoja na kumsindikiza kliniki ili kupata maelekezo muhimu kutoka kwa wataalamu wa afya.

“Baba ni mfanya maamuzi katika familia, hivyo anapopata taarifa sahihi moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa afya inasaidia sana katika kuhakikisha mama na mtoto wanapata huduma sahihi wakati wa ujauzito na hata baada ya kujifungua,” alisema.

Katika mdahalo huo pia walikuwepo viongozi mbalimbali wa serikali na jamii akiwemo Mtendaji wa Kata ya Shagihilu Simoni Lue, ambaye alisimamia zoezi la kuweka maazimio ya pamoja ya jamii.

Baadhi ya makubaliano yaliyofikiwa katika mdahalo huo ni pamoja na:

  • Wababa kujitolea kuwasindikiza wake zao kliniki wakati wa ujauzito na wakati wa huduma za afya.
  • Wanaume kuacha hofu ya kupima afya zao na kujitokeza hospitalini kwa ajili ya uchunguzi wa afya.
  • Jamii kuachana na mila na mitazamo inayozuia wanaume kushiriki katika masuala ya afya ya familia.
  • Wababa kutoa msaada wa karibu kwa wake zao wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.
  • Wanajamii kuendelea kupokea na kusambaza elimu ya afya ili kulinda maisha ya mama na mtoto.
  • Vikundi vya Baba Bora kuendelea kutoa elimu kwa wanaume wengine katika jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki katika afya ya familia.

 

Diwani wa Kata ya Shagihilu Deogratius Nicas pia alitoa hamasa kwa wananchi hasa wanaume kushiriki kikamilifu katika masuala ya afya ya mama na mtoto.

Alisisitiza kuwa ushiriki wa baba ni muhimu katika kulinda afya ya familia na kujenga jamii yenye ustawi.

Mdahalo huo umeacha mwamko mpya kwa wananchi wa Shagihilu ambapo wanaume wameahidi kuongeza ushiriki wao katika huduma za afya ili kuhakikisha mama na mtoto wanapata uangalizi bora na kupunguza hatari ya vifo vinavyoweza kuzuilika.

 

Kupitia mradi wa Grow ENRICH, shirika la Kivulini pamoja na World Vision wanaendelea kuimarisha ushirikiano na jamii ili kuhakikisha kila familia inapata elimu na huduma bora za afya kwa maendeleo endelevu ya jamii.

Meneja mradi kutoka Shirika la Kivulini, Mageni Malulu akizungumza.

Afisa maendeleo Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Lailat Ramadhani akizungumza.Afisa lishe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Bwana Amrani Idd akizungumza.









Post a Comment

Previous Post Next Post