" SHUKRANI GIDEON APONGEZWA KWA KUWALEA VIZURI WATOTO YATIMA MBEYA

SHUKRANI GIDEON APONGEZWA KWA KUWALEA VIZURI WATOTO YATIMA MBEYA


Na Lydia Lugakila-Misalaba Media 

Mbeya 

“Asingekuwa huyu Mama Shukrani Gideon, sijui hawa watoto yatima wangekuwa wapi?”

Haya ni maneno ya baadhi ya akina mama wafanyabiashara wa Mkoa wa Mbeya walioungana na Bi. Shukrani Gideon katika tukio la kugawa misaada na kushiriki chakula pamoja na watoto yatima wa Shule ya Sekondari Vanessa, iliyopo Isyesye, jijini Mbeya.

Tukio hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) pamoja na Siku ya Mwanamke Duniani mwaka 2026, ambapo badala ya kufanya sherehe, wanachama hao waliamua kugusa maisha ya wahitaji

Mwenyekiti wa TWCC Mkoa wa Mbeya, Bi. Rehema Robert alisema kuwa  waliona ni vyema kusherehekea kwa kutoa msaada kwa watoto yatima badala ya kujifanyia sherehe wenyewe. 

Katika tukio hilo, walikabidhi magodoro, unga pamoja na nguo kwa watoto hao.

Bi. Rehema alimpongeza Bi. Shukrani Gideon kwa juhudi zake kubwa na za muda mrefu katika kuwalea na kuwasaidia watoto yatima, akisema ni mfano wa kuigwa katika jamii.

Aidha, mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa chama hicho kitaendelea kuwajali watoto yatima ili waweze kutimiza ndoto zao za kielimu, huku akitoa wito kwa walezi kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi bora.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bi. Shukrani Gideon, ambaye ni mmiliki wa Shule ya Sekondari Vanessa chini ya Tehirah Foundation, alisema tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 2006, lengo kuu lilikuwa kusaidia watoto yatima na wale wanaotoka katika mazingira hatarishi.

Alisema kuwa katika kuadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, wamepokea ugeni kutoka TWCC Mkoa wa Mbeya ambao wameguswa na maisha ya watoto 66 waliopo shuleni hapo na kutoa msaada wa magodoro 30.

Bi. Gideon alibainisha kuwa kuanzia mwaka 2006 hadi 2026, wamefanikiwa kuwasaidia watoto 1,029 kusoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, huku wengine wakifanikiwa kufika elimu ya juu vyuoni.

Aliongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri wa jamii pamoja na Serikali kupitia idara mbalimbali, ikiwemo ustawi wa jamii, ambao husaidia kuwabaini watoto wenye uhitaji na kuwaunganisha na taasisi hiyo.

Kutokana na baadhi ya watoto kubaki shuleni wakati wa likizo kwa kukosa pa kwenda, Bi. Gideon amesema ana mpango wa kujenga nyumba maalum kwa ajili yao ili waweze kuwa na makazi salama wakati wa mapumziko.

Alibainisha kuwa watoto wanaohudumiwa wanatoka maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Mbeya, Dodoma, Dar es Salaam na Singida.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Tehirah Foundation, Bw. Zephania Gideon, alisema kuwa taasisi hiyo inawaweka pamoja watoto yatima na wasiokuwa yatima ili kuepusha ubaguzi na kuwajengea hali ya kujiamini.

Aliongeza kuwa watoto yatima wanapatiwa mahitaji yote muhimu ikiwemo ada, chakula, sare za shule pamoja na mahitaji binafsi.

Zephania  alisema kuwa watoto 824 wamehitimu kidato cha nne, 187 kidato cha sita, na 13 wamefanikiwa kusoma katika vyuo vikuu na vyuo vya kati. Pia, baadhi ya wahitimu wa kidato cha nne wamewezeshwa mafunzo ya ujasiriamali kupitia SIDO.

Mwenyekiti wa TWCC Mkoa wa Mbeya Bi Rehema Robert

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post