" VIJANA SHINYANGA WALIA NA UKOSEFU WA AJIRA, WAIOMBA SERIKALI KUWAWEZESHA

VIJANA SHINYANGA WALIA NA UKOSEFU WA AJIRA, WAIOMBA SERIKALI KUWAWEZESHA

Na Edington Mukiza Ezron, Misalaba Media

Baadhi ya vijana katika Manispaa ya Shinyanga wameiomba serikali kuwawezesha kwa kuwapatia fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo mikopo yenye masharti nafuu, zabuni, pamoja na kushirikishwa katika miradi ya maendeleo ili waweze kujipatia kipato na kujikwamua kimaisha.

Wakizungumza na Misalaba Media leo Machi 27, 2026 katika nyakati tofauti, vijana hao wameeleza kuwa changamoto ya ukosefu wa ajira bado ni kubwa, na kwamba hali hiyo inahitaji juhudi za pamoja kati ya serikali na jamii kwa ujumla ili kuipunguza na hatimaye kuimarisha maisha ya vijana.

Mmoja wa vijana hao, Zephania Tulinge Lucas, mkazi wa Kata ya Ngokolo, amesema ukosefu wa ajira umesababisha baadhi ya vijana kujiingiza katika vitendo visivyofaa ikiwemo wizi, matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kukata tamaa ya kuendelea na masomo kutokana na kutokuona manufaa ya elimu.

Kwa upande wake, Joseph Steven amesema serikali haina budi kuongeza uwekezaji utakaosaidia kutoa ajira kwa vijana, pamoja na kuweka mikopo yenye riba nafuu ili kuwawezesha kuanzisha na kuendesha biashara zao.

Aidha, amewashauri vijana kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kujipatia kipato badala ya kusubiri ajira rasmi, ili waweze kuendesha maisha yao.

Naye Magreth Charles Marwa amesema vijana wanapaswa kuwa wabunifu na kutojikita tu kwenye elimu waliyonayo, bali kutafuta fursa mbalimbali zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi na kuepuka kujiingiza katika vitendo vya uhalifu.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa serikali kuweka mazingira rafiki kwa vijana kwa kutoa ajira ndogo ndogo, mikopo ya biashara pamoja na elimu ya ujasiriamali.

Hata hivyo, amewataka vijana wasio na ajira kuwa wavumilivu huku wakijishughulisha na shughuli mbalimbali wanazosubiri fursa za ajira serikalini, ili waweze kutimiza ndoto zao.

Aidha, vijana hao wameeleza kuwa licha ya kuwepo kwa mikopo na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali, bado elimu kuhusu upatikanaji na taratibu zake haijawafikia moja kwa moja, hali inayowafanya wengi kushindwa kunufaika na fursa hizo kutokana na ukosefu wa taarifa sahihi.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post