
Na John Walter-Babati
Tukio la kusikitisha limeutikisa wakazi wa eneo la Magugu, wilayani Babati mkoani Manyara, baada ya mwili wa mwanaume ambaye bado hajatambulika kukutwa umetupwa pembeni mwa barabara kuu ya Babati–Arusha.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, marehemu ana dalili za kuuawa kikatili, huku chanzo cha tukio hilo kikiwa bado hakijabainika.
Wananchi wa eneo hilo wameeleza hofu kubwa kufuatia tukio hilo, wakihofia usalama wao na kuziomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kuwabaini wahusika na kuimarisha ulinzi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Magugu, Lohay Amos, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akieleza kuwa limetokea usiku wa kuamkia Machi 19 katika eneo la Kwa Chami.
Amesema mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa na majeraha makubwa kichwani, ambapo inaelezwa kuwa alipigwa na kitu kizito kinachofanana na shoka, hali iliyosababisha kuharibika kwa taswira ya uso na kufanya kuwa vigumu kutambulika.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Magugu huku uchunguzi ukiendelea.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Babati, Mrakibu wa Polisi Ernesta Mwambinga, alifika eneo la tukio na kuwahakikishia wananchi kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliohusika na tukio hilo la kinyama.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zozote zitakazosaidia uchunguzi, akisisitiza kuwa taarifa hizo zitahifadhiwa kwa siri.
Wananchi wa Magugu wamelalamikia kuongezeka kwa matukio ya ukatili katika eneo hilo, wakitaka ulinzi uimarishwe pamoja na uwekaji wa taa za barabarani, hasa katika maeneo yenye giza nene nyakati za usiku.
Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada za kumtambua marehemu na kubaini ukweli wa tukio hilo.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment