" TRA YAPANIA KUIFUNGA MSIMBAZI ‘SIMBA’ MBELE YA MASHABIKI WAKE ARUSHA

TRA YAPANIA KUIFUNGA MSIMBAZI ‘SIMBA’ MBELE YA MASHABIKI WAKE ARUSHA

Na  Bora Mustafa, Arusha.

Timu ya wakusanya kodi chini ya TRA imejipanga kuendeleza ubabe wake katika nyasi za nyumbani wakati itakaposhuka dimbani leo kuwakabili wekundu wa Msimbazi “Simba” katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaopigwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari machi 13,2026 , msemaji mkuu wa Klabu ya TRA, Christina Mwagala, amesema timu yao imejiandaa kikamilifu kuhakikisha inaibuka na ushindi katika mchezo huo wa nyumbani.

 Pia amesema kuwa kikosi hicho kimeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kinawazuia Simba kupata ushindi, huku wakilenga kutumia vyema faida ya kucheza mbele ya mashabiki wao wa Arusha.

Christina Mwangala, Afisa Habari TRA FM

“Tunajua Simba ni timu nzuri na yenye uzoefu mkubwa, lakini hatuwaogopi. Tumejiandaa vizuri na tunaamini mashabiki wetu watatuunga mkono ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema Mwagala.

Aidha, ameongeza kuwa matokeo ya ushindi katika mechi za nyumbani yameiwezesha TRA kupanda hadi nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC, tofauti na awali walipokuwa nafasi ya kumi na mbili kabla ya kushinda michezo kadhaa iliyopita.

Pamoja na hayo, Mwagala ameeleza kuwa mchezo wa leo ni muhimu kwa timu yao kwani ushindi utaimarisha nafasi yao kwenye msimamo wa ligi na kuwapa morali ya kuendelea kupambana katika michezo inayofuata.

 Aidha amesema Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, huku mashabiki wa soka jijini Arusha wakisubiri kwa hamu kuona kama TRA itaweza kuizuia Simba kupata ushindi au kama wekundu hao wa Msimbazi wataibuka na pointi muhimu ugenini.

Post a Comment

Previous Post Next Post