Ushauri uliotolewa na Emelian Busara unalenga kubadili mtazamo wa Watanzania waishio nje kutoka kwenye kutuma fedha za matumizi ya kawaida kuelekea kwenye uwekezaji wa kimkakati unaozalisha faida ya muda mrefu.
Masoko ya mitaji, ambayo yanajumuisha ununuzi wa hisa katika makampuni yaliyoorodheshwa na uwekezaji katika hati fungani za serikali, yanatajwa kuwa njia salama zaidi kwa sababu yanasimamiwa na sheria kali na mamlaka za kiserikali zinazohakikisha uwazi.
Kwa mwananchi aliye nje ya nchi, changamoto kubwa imekuwa ni namna ya kusimamia mali zake bila kuhitaji uwepo wake wa kimwili, na hapa ndipo soko la hisa linapokuja kama suluhu ya kudumu kwani fedha inafanya kazi yenyewe kupitia mfumo wa kidijitali.
Tukitazama nchi nyingine duniani, tunaona jinsi mataifa kama Ethiopia na India yalivyotumia masoko ya mitaji kuimarisha uchumi wao kupitia nguvu ya Diaspora.
Kwa mfano, Serikali ya Ethiopia ilifanikiwa kukusanya mamilioni ya dola kutoka kwa raia wake waishio nje kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la "Great Renaissance" kupitia hati fungani maalum, jambo lililowapa wawekezaji hao riba ya uhakika huku wakichochea maendeleo ya nchi yao.
Nchini Philippines, mfumo wa soko la mitaji umefungamanishwa na teknolojia kiasi kwamba mfilipino aliyeko Marekani anaweza kununua hisa za makampuni ya nyumbani kwao kupitia simu yake ya mkononi, hatua inayopunguza utegemezi wa ndugu na marafiki katika usimamizi wa fedha.
Umuhimu wa uwekezaji huu kwa Mtanzania waishio nje ni mkubwa kwani unampa kinga dhidi ya mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya fedha kulinganisha na kuacha fedha hiyo kwenye akaunti ya akiba ya kawaida. Aidha, uwekezaji katika hati fungani za serikali unatoa uhakika wa malipo ya riba kila baada ya miezi sita, jambo ambalo ni muhimu sana kwa mtu anayepanga kustaafu na kurejea nyumbani akiwa na chanzo cha mapato kisichoyumba.
Teknolojia sasa inaruhusu wawekezaji hawa kuona mienendo ya mitaji yao na kupokea gawio lao moja kwa moja kwenye akaunti zao, jambo ambalo linaimarisha imani na kuongeza ushiriki wa mwekezaji mmoja mmoja katika kukuza uchumi wa taifa.
Mwisho, uwekezaji huu ni chachu ya maendeleo ya kitaifa kwa sababu unatoa ukwasi kwa makampuni ya ndani na serikali kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu kama barabara, reli, na nishati. Diaspora wanapowekeza kwenye soko la hisa, wanakuwa wamiliki wa sehemu ya uchumi wa nchi yao na wanapata fursa ya kufaidika na ukuaji wa sekta za kibenki, mawasiliano, na madini. Hii inajenga uhusiano wa kifaida kati ya mwekezaji na nchi yake, ambapo mwekezaji anapata utajiri wa binafsi huku nchi ikipata mtaji wa ndani wa kujiendesha bila kutegemea mikopo ya nje yenye masharti magumu.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment