Katika kile kinachoonekana kuwa ni mkakati wa makusudi wa kuitumia nguvu kazi ya vijana nchini, Serikali imezindua Programu ya Mafunzo kwa Wawekezaji Vijana na Kituo cha Pamoja cha Kuwezesha Manunuzi na Mauzo ya Nje (Sourcing and Export Center).
Uzinduzi huo uliofanyika Machi 14, 2026, katika Eneo Maalum la Kiuchumi la B.W. Mkapa (Mabibo SEZ), jijini Dar es Salaam na unalenga kuwajengea uwezo vijana wa Kitanzania kuwa sehemu ya mnyororo wa uzalishaji wa bidhaa za viwanda zenye ubora wa kimataifa.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amebainisha kuwa asilimia 80 ya Watanzania wana umri wa chini ya miaka 40, jambo linalofanya kundi hilo kuwa injini kuu ya uchumi.
Prof. Mkumbo amesisitiza kuwa tofauti na nchi za Ulaya na Asia zinazokimbilia teknolojia ya roboti kutokana na uhaba wa vijana, Tanzania inawekeza kwa watu wake ili kuendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga rasilimali watu yenye ujuzi wa hali ya juu na ushindani wa biashara nje ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri, ameeleza kuwa programu hiyo ni ya kipekee kwani washiriki hawatajifunza darasani pekee, bali watahusika moja kwa moja na uzalishaji katika hali halisi ya viwandani. Awamu ya kwanza itahusisha vijana 30 hadi 50 watakaofundishwa uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo yanayokaushwa kwa ajili ya soko la ndani na nje. Aidha, vijana hao watatumia miundombinu ya pamoja (Production Shared Facilities) ili kupunguza gharama za uwekezaji.
Moja ya mafanikio makubwa ya programu hiyo ni ushirikiano uliopatikana nchini China (Jimbo la Zhejiang) kufuatia ziara ya Prof. Kitila Mkumbo mwishoni mwa mwaka jana. Kupitia ushirikiano huo, TISEZA imepata mbia wa kwanza atakayesaidia wawekezaji vijana katika manunuzi ya mitambo na vifaa vya kisasa kutoka China (Sourcing), huku akitoa huduma ya uhakiki wa wasambazaji ili kuzuia matapeli wa kimataifa.
Kituo hicho cha pamoja kitakuwa suluhu ya kudumu kwa kutoa huduma jumuishi ikiwemo uhakiki wa vigezo vya kisheria vya masoko ya nje, usimamizi wa mizigo na ugavi, pamoja na kuunganisha vijana wanaochipukia na wafanyabiashara wakubwa (Mentorship).
Kwa hatua hii, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaonyesha dhamira ya wazi ya kuifanya sekta ya uwekezaji kuwa jumuishi, ikiwapa vijana fursa ya kuwa wamiliki wa viwanda badala ya kuwa wafanyakazi pekee.
Hii ni hatua ya "Kupindua Meza." Kwa muda mrefu vijana wamekuwa wakilalamika kuhusu mitaji na teknolojia, lakini kituo hiki kinakuja na suluhu ya pamoja. Uwepo wa mbia kutoka China wa kurahisisha ununuzi wa mitambo ni habari njema sana kwa vijana wajasiriamali ambao walikuwa wakipata tabu ya kutapeliwa au kupata mitambo isiyo na viwango.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment