Na Edington Mukiza Ezron, Misalaba Media
Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Shinyanga
wamewahimiza vijana kutumia mitandao ya kijamii kama nyenzo ya kujikwamua
kiuchumi na kuchangamkia fursa mbalimbali za maendeleo zinazopatikana kupitia
majukwaa hayo.
Wakizungumza na Misalaba Media kwa nyakati tofauti leo
Machi 31, 2026, wananchi hao wamesema matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii
yanaweza kuwa chachu ya maendeleo kwa vijana endapo yatatumika kwa malengo
chanya.
Mmoja wa wananchi hao, Grace Yona, amesema vijana
wanapaswa kuitumia mitandao ya kijamii kujiimarisha katika sekta mbalimbali
ikiwemo biashara, elimu, sanaa na michezo, badala ya kuitumia kwa mambo yasiyo
na tija.
Ameongeza kuwa kupitia mitandao ya kijamii, vijana
wanaweza kujenga mahusiano mapana na watu mbalimbali, jambo linaloweza
kuwasaidia kupata fursa na kuongeza kipato.
Kwa upande wake, Yusufu Michael amesema baadhi ya
vijana wamekuwa wakitumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuiga tamaduni
zisizofaa na kujihusisha na vitendo vinavyokiuka maadili ya Kitanzania, hali
inayochangia mmomonyoko wa maadili katika jamii.
Aidha, amesisitiza kuwa wazazi pamoja na serikali
wanapaswa kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kuwasaidia
vijana kuelewa umuhimu wake na kuepuka matumizi yasiyofaa.
Naye Yohana Edward amesema baadhi ya vijana wamekuwa
wakijihusisha na vitendo vya uhalifu kama wizi, utapeli pamoja na kusambaza
maudhui yasiyofaa mtandaoni, jambo ambalo linaweza kuathiri mustakabali wao na
kuwafanya wakumbwe na hatua za kisheria.
Kwa upande mwingine, baadhi ya vijana wameiomba
serikali kuboresha upatikanaji wa huduma za intaneti kwa gharama nafuu,
wakisema gharama za vifurushi vya data ni kubwa na zinawazuia kutumia ipasavyo
fursa zilizopo mtandaoni.
Hata hivyo, vijana wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa uangalifu na malengo yenye tija, ili kuepuka kuharibu maadili, kuchafua sifa zao pamoja na kujiepusha na athari za kisheria zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi mabaya ya teknolojia hiyo.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment