Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii wameishauri Serikali kuhakikisha kuwa vijana wanaohitimu mafunzo kupitia Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi (Uanagenzi) hawaachwi njiani, bali wanawezeshwa kwa mitaji na masoko ili waweze kujiajiri.
Wabunge hao wamesisitiza kuwa lengo kuu la programu hiyo ni kuwajengea vijana stadi shindani zinazowawezesha kujitegemea badala ya kusubiri kuajiriwa, huku wakitaka kuwepo kwa utaratibu mahsusi wa serikali wa kuunganisha bidhaa na huduma za vijana hao na walaji ili kuleta tija kwa taifa.
Katika michango yao, baada ya kutembelea Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kigamboni, Machi 16,2026 , kusikiliza wanagenzi na hoja zao wabunge wamependekeza kuanzishwa kwa ‘makongano’ (industrial clusters) ambapo wahitimu hao watawekwa katika maeneo maalum yanayofahamika, hali itakayowasaidia kuratibiwa kwa urahisi na kuwawezesha wateja kuwapata kwa urahisi.
Akizungumzia umuhimu wa kunoa weledi, Mbunge Kangi Lugola amelinganisha programu hiyo na juhudi za zamani za NIP, akisisitiza kuwa ni lazima kuwepo na mpango madhubuti wa kuendeleza ujuzi huo ili wahitimu wasibaki mitaani bila kazi. Aidha, kumejitokeza hoja ya kuwataka mafundi magari wanaofundishwa katika vyuo hivyo kupewa pia mafunzo ya udereva ili waweze kumudu majaribio ya vyombo wanavyotengeneza na kuongeza ushindani wao sokoni.
Kwa upande wake, Mbunge anayewakilisha watu wenye ulemavu ameipongeza Serikali kwa kuwajumuisha wenye mahitaji maalum katika programu hiyo na kushauri vyuo vya maendeleo ya wananchi kuanzisha vitengo vya kilimo na ufugaji wa kisasa. Wakati huo huo, Mbunge wa Temeke amehimiza chuo hicho kujitangaza zaidi ili jamii ifahamu fursa zilizopo, huku akimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kuwafikia wananchi wa hali ya chini na kuhakikisha wanafaidika na rasilimali za nchi.
Hoja nyingine nzito iliyoibuliwa ni hitaji la kutambuliwa kwa vyeti vya wahitimu hao katika mifumo rasmi ya kielimu na ajira. Mbunge Jumanne amebainisha kuwa kwa sasa wahitimu wanakabiliwa na changamoto ya vyeti vyao kutotambulika kisheria, jambo linalokwamisha maendeleo yao. Wabunge pia wamehimiza Serikali kuongeza bajeti ya vyuo hivyo ili viweze kununua vitendea kazi na vifaa vya kisasa vya kiteknolojia, wakionya kuwa kutoa elimu ya kizamani kutaacha vijana nyuma ya wakati.
Akijibu hoja hizo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mheshimiwa Deus Sangu, amepokea ushauri huo na kuahidi kuwa wizara itaagiza vyuo vyote vinavyofundisha ufundi magari kujumuisha mafunzo ya udereva. Waziri Sangu ameeleza kuwa atafanya mazungumzo na Waziri anayehusika na masuala ya vijana ili kuweka mpango wa uwezeshaji kupitia mikopo na ruzuku. Amekubali pia umuhimu wa kuingiza teknolojia mpya akitolea mfano wa madereva waliokwenda Qatar, ambao mafanikio yao yalitegemea uwezo wa kutumia mifumo ya kisasa kama GPS.
Akifunga mjadala huo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ameitaka Serikali kuhakikisha ushauri wa wabunge wa kuongeza wigo wa udahili, kuimarisha bajeti, na kuhakikisha vyeti vinatambulika unatekelezwa kikamilifu. Amesisitiza kuwa kuimarisha mafunzo hayo na kuwapa wahitimu zana za kisasa ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kizazi cha sasa kinanufaika na programu hiyo na kuwaepusha vijana kuwa "mafundi njaa" mitaani.
Awali wanufaika wa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi (Uanagenzi) katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Kigamboni, wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia mitaji na vifaa vya kazi mara wanapohitimu ili waweze kutumia ujuzi wao kujiajiri. Ombi hilo limetolewa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, ambapo vijana hao walieleza kuwa licha ya kupata ujuzi wa hali ya juu, changamoto ya vyeti vyao kutotambulika katika mifumo rasmi ya kielimu na ukosefu wa nyenzo za kuanzia maisha, inakwamisha kasi yao ya maendeleo.
Mmoja wa wanufaika hao, Husna Hamisi, ambaye kwa sasa amefanikiwa kupata ajira, amebainisha kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa Serikali kuandaa utaratibu wa mikopo ya vifaa au mitaji kwa vijana wanaomaliza mafunzo hayo. Husna amesisitiza kuwa kijana anapohitimu bila kuwa na nyenzo za kazi, anajikuta akishindwa kutekeleza kile alichojifunza, hali inayofifisha malengo ya programu hiyo. Aidha, aligusia kero ya vyeti akisema kuwa kutotambulika kwake katika mfumo rasmi kunawanyima fursa nyingi za ushindani katika soko la ajira na kujiendeleza kimasomo.
Kauli hiyo imeungwa mkono na Elia, mnufaika mwingine ambaye ameitaja programu hiyo kuwa ndiyo siri ya mafanikio yake ya sasa. Elia ameeleza kuwa ujuzi aliopata umemthibitishia kuwa "ujuzi ni ajira" na umempa heshima katika jamii, akiiomba Serikali isiwache njiani wahitimu hao bali iwawezeshe ili wasikae bila kazi mitaani. Shukurani za pekee zimetolewa pia na wazazi, ambapo Flora Paschal, mwenye mtoto anayesoma chuoni hapo, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka vijana wa hali ya chini. Flora amesema kuwa bila programu hiyo, vijana wengi wangekuwa wakizurura mitaani na kujiingiza katika makundi yasiyo na maadili.
mwisho
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment