TAARIFA KWA UMMA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kuimarisha
ulinzi na usalama wa raia na mali zao kwa kufanya misako na doria katika maeneo
mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya hali inayopelekea Amani na Utulivu.
Tarehe
25.03.2026 kati ya saa 6 hadi saa 9:30 usiku katika Kata ya Nkunga, Lupepo, Kawetele
na Ikuti Wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya, mvua kubwa iliyoambatana na upepo
ilinyesha na kusababisha vifo vya watu 18 kati yao watu wazima ni 04 [wanawake
3 na mwanaume 1] na watoto waliofariki dunia ni 14 [wa kike 8 na wa kiume 6].
Mvua hiyo
iliyoambatana na upepo mkali ilisababisha nyumba zaidi ya 9 zilizojengwa kwa
tofali mbichi na kuezekwa bati kusombwa na maporomoko ya udongo mzito na
kusababisha vifo hivyo. Walifariki katika maafa hayo ni Chapakazi Mwasota [60],
Rhoida Mwangwina [55], Gladness Chapakazi [18], Neema Mwasyema [31], Aneth
Morohan [35], Obeid Shibuka [20] na Itika Manyanya [26].
Watoto waliofariki
katika Maafa hayo ni Vivian Ahonga, mwaka 1, Briana Mwachiombo [3], Dailan
Kasambala [6] aliyekuwa Mwanafunzi wa Chekechea katika Shule ya Msingi Lupepo, Innoent
Kasambala [4], Vivian Andrea [13] aliyekuwa Mwanafunzi Darasa la Saba katika
Shule ya Msingi Lupepo, Princess Ibrahim [5] aliyekuwa Mwanafunzi wa Chekechea
katika Shule ya Msingi Lupepo, Nathanael Christopher [2], Jonathan Hamis, miezi
kumi, Irine Anangisye [16] aliyekuwa Mwanafunzi wa Kidato cha Tatu katika Shule
ya Sekondari Lupepo, Wema Hamis [5] aliyekuwa Mwanafunzi wa Chekechea katika
Shule ya Msingi Kikuyu na Kenedy Mahenge [14], aliyekuwa Mwanafunzi wa Kidato
cha Pili Sekondari ya Ikuti.
Aidha,
katika Maafa hayo watu 5 walijeruhiwa kati yao watoto 3 wa kike na watu wazima 2,
mwanaume 1 na mwanamke 1. Majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu katika
Hospitali ya Wilaya Makandana – Tukuyu na Zahanati ya Chuo cha Magereza Kiwira.
Jeshi la
Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji
linaendelea na kazi ya Uokoaji katika maeneo hayo. Aidha, timu za Madaktari
zipo maeneo hayo kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kitabibu wa miili ya
marehemu na kutoa huduma za awali kwa wahanga. Kamati ya Maafa ya Wilaya pia
inaendelea na tathimini ya matukio hayo na kutoa misaada kwa wahanga wengine
wakazi wa maeneo hayo.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
linamshikilia Gilbert Edwin Mwabulesi [26] mkazi wa Ibililo Wilayani Rungwe
Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma za mauaji ya baba yake mzazi aitwaye Edwin Mwabulesi
[65] aliyekuwa mkazi wa Kijiji cha Ibililo kwa kumpiga sehemu mbalimbali za
mwili.
Tukio hilo lilitokea Machi 21, 2026 saa 9:20 usiku
katika Kitongoji cha Nsanga, Kijiji cha Ibililo, Kata ya Nkunga, Tarafa ya
Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya baada ya mtuhumiwa Gilbert Mwabulesi
kumshambulia kwa kumpiga ngumi na mateke sehemu mbalimbali za mwili baba yake
mzazi aitwaye Edwin Mwabulesi na kusababisha kifo chake.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio ni
mzozo wa kifamilia uliotokea baina yao ambapo mtuhumiwa anaishi na wazazi wake,
hivyo baada ya kurudi kutoka matembezini alianza kugonga mlango kwa fujo
akipiga kelele na kutokana na vitendo hivyo baba yake mzazi aliamka na kumfuata
kwa lengo la kumuonya ndipo alianza kumshambulia kwa kumpiga hadi kufariki
dunia.
Taratibu za kisheria zinakamilishwa ili mtuhumiwa
afikishwe mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa
wananchi kuchukua tahadhari kipindi hiki cha mvua za masika zinazoendelea
kunyesha katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya ili kuepuka madhara. Aidha,
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa baadhi ya vijana kuacha matumizi
ya dawa za kulevya na kupelekea kufanya uhalifu.
imetolewa na:
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment