Farida Mangube Morogoro
Watu watatu wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia ajali ya kugongana uso kwa uso kati ya lori na basi iliyotokea Aprili 21, 2026 majira ya asubuhi mkoani Morogoro.
Ajali hiyo ilitokea katika eneo la kona S, kitongoji cha Kikoni, kijiji cha Lumango, kata ya Kidodi, wilayani Kilosa barabara kuu ya Mikumi–Kilombero.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi la Polisi ajali hiyo ilihusisha lori aina ya FAW lenye namba za usajili T154 ECP/T229 EBY lililokuwa likiendeshwa na Yasin Omary Nasiri (48), mkazi wa Dar es Salaam, pamoja na basi la kampuni ya ZL Super lenye namba T996 EPP lililokuwa likiendeshwa na Emanuel Benito.
Inadaiwa kuwa dereva wa lori alijaribu kulipita pikipiki ya magurudumu matatu (Toyo) iliyokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari, hali iliyosababisha kugongana uso kwa uso na basi hilo lililokuwa likitoka Ifakara kuelekea Dodoma.
Waliofariki katika ajali hiyo ni dereva wa lori, Yasin Omary Nasiri (48), pamoja na Awadhi Ngwanda (60) na Zalaph Awadhi Ngwanda (20), wakazi wa Mang’ula.
Aidha, waliojeruhiwa ni pamoja na mwanaume mmoja ambaye bado hajafahamika jina lake mwenye umri wa kati ya miaka 40 hadi 45.
Wengine ni Amani Iddi (60), mkulima mkazi wa Ifakara; Matha John (39), mfanyabiashara mkazi wa Dodoma; Pendo Kui (68), mkulima mkazi wa Singida; na Monica Lameck Mazuwameli (16), mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Iwemba, mkazi wa Lumango.
Majeruhi wote wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya St. Kizito iliyopo Mikumi.
Aidha jeshi la Polisi limewataka madereva na watumiaji wa barabara kuzingatia sheria na alama za barabarani ili kuepusha ajali, likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka sheria hizo.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment