
NA DENIS MLOWE, IRINGA
JESHI la Polisi Mkoa wa Iringa limeendelea na operesheni za kuzuia uhalifu kwa lengo la kuhakikisha usalama wa raia na mali zao, na kufanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa wawili wanaodaiwa kuwa viongozi wa mtandao wa utapeli kupitia kampuni za Alliance in Motion Global na Q-NET.
Akizungumza na wanahabari Kamanda wa Jeshi la Polisi .Mkoa Iringa Sacp Allan Bukumbi aliwataja Watuhumiwa hao ni Jackson Kalu (26), mjasiriamali mkazi wa Bahi mkoani Dodoma na Michael Mfuse (32), mkazi wa Wanging’ombe mkoani Njombe. Mfuse alikamatwa akiwa na gari lenye namba za usajili T1G6EMJ aina ya BMW X1 ambalo inadaiwa lilitumika katika shughuli za uhalifu huo pamoja na kupatikana na nyaraka mbalimbali zinazohusishwa na kampuni ya Q-NET.
Alisema kuwa Katika operesheni hiyo, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuokoa wahanga 75 wa mtandao huo, wakiwemo wanawake 36 na wanaume 39, ambao walikuwa wakidanganywa kwa ahadi za ajira ndani na nje ya Tanzania.
Bukumbi alisema kuwa Wahanga hao, ambao wengi wao ni vijana wenye umri kati ya miaka 20 hadi 30, wanatoka mikoa ya Dodoma, Mwanza, Lindi, Njombe, Mtwara pamoja na Mafia.
Imeelezwa kuwa viongozi wa genge hilo wamekuwa wakiwalaghai vijana hao kwa madai ya kuwatolea ajira kupitia kampuni zao, kisha kuwataka wafike mkoani Iringa kwa hatua za kuanza kazi au safari kuelekea nje ya nchi. Baada ya kufikishwa Iringa, vijana huanza kufundishwa na kupewa masharti ya kuwasilisha kiasi cha fedha kati ya shilingi 600,000 hadi 4,000,000 kutoka kwa wazazi au walezi, wakidai kuwa fedha hizo ni ada, usajili na kiingilio cha biashara.
Aidha, huambiwa kuwa mtu atakayeleta wafuasi wawili atarejeshewa fedha zake pamoja na mtaji wa biashara.
Uchunguzi umebaini kuwa vijana hao wamekuwa wakiishi katika mazingira yasiyofaa, ambapo zaidi ya watu 10 hulazimika kulala katika chumba kimoja wakati wakisubiri kuanza shughuli hizo haramu, jambo linalokiuka sheria na kanuni za nchi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limewataka wazazi na walezi ambao watoto wao waliondoka majumbani kwao kwa ahadi za ajira na hawajulikani walipo kufika Kituo Kikuu cha Polisi Iringa ili kuwatambua vijana waliookolewa.
Aidha, jeshi hilo limewataka wazazi kuwafuatilia na kuwasimamia kwa karibu watoto wao ili kuepusha kutapeliwa au kujiingiza katika vitendo vya kihalifu.
Katika hatua nyingine, kuelekea Sikukuu ya Pasaka itakayofuatiwa na maadhimisho ya Karume Day, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuchukua tahadhari, hususan wazazi na walezi kuhakikisha usalama wa watoto. Pia, watumiaji wa vyombo vya moto wametakiwa kufuata sheria na alama za barabarani ili kuepusha ajali.


SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment