" MAFUNZO YA “SAFARI YA MPAJI UZIMA” YAHITIMISHWA SHINYANGA

MAFUNZO YA “SAFARI YA MPAJI UZIMA” YAHITIMISHWA SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba


Mafunzo ya siku nne ya program ya Safari ya Mpaji-Uzima yamefanyika katika ukumbi uliopo Kata ya Ndala, Manispaa ya Shinyanga, yakilenga kuwajengea uwezo viongozi wa dini na wadau mbalimbali kuhusu thamani ya maisha ya mwanadamu na masuala ya kiroho yanayohusiana na uhai.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Shirika la Lifeline Cocenselly Centre and Gender Empowerment, Dkt. Meshack Kulwa, amesema kuwa program ya Safari ya Mpaji-Uzima ni sehemu ya miradi ya taasisi ya Life International yenye makao yake nchini Marekani, ambayo ilianzishwa kwa lengo la kupinga utoaji mimba na kulinda uhai wa binadamu.

Amesema Lifeline imefanikiwa kuanzisha ushirikiano na taasisi hiyo baada ya mawasiliano ya takribani miaka mitatu, hatua iliyowezesha kuanza rasmi utekelezaji wa program hiyo nchini Tanzania.

“Tumekuja na safari ya mpaji uzima kwa ajili ya kutengeneza uelewa kwa jamii, na baadaye tutaweka mazingira ya kuwafikia Watanzania wengi zaidi. Huu ni mwanzo tu, lakini tuna mipango mingine”amesema Dkt. Kulwa.

Ameongeza kuwa semina hiyo imewakutanisha washiriki kutoka maeneo mbalimbali nchini, wakiwemo viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu, akiwataja wachungaji, maaskofu na masheikh kutoka mikoa ya Geita, Tabora, Dodoma, Shinyanga na Dar es Salaam. Pia mafunzo hayo yamewezeshwa na wakufunzi kutoka Nairobi nchini Kenya.

Dkt. Kulwa amewasisitiza washiriki kutumia elimu waliyoipata kwa vitendo katika jamii zao, akiwahimiza kuanzia kwenye nyumba za ibada na taasisi wanazozisimamia ili kufikisha ujumbe mpana zaidi kwa jamii.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya wawezeshaji kutoka Nairobi, Mtume Patrick Ngundo amesema mafunzo hayo ni ya muhimu kwa washiriki kwani wao ndio waliobeba dhamana ya kuifikisha elimu hiyo kwa wengine.

“Hili tulilopokea ni muhimu sana. Sisi tumewapa elimu na tunatarajia mkaifikishe kwa wengine kule ambako hatuwezi kuwafikia. Huu ni mwanzo wa safari, na kwa msaada wa Mungu tutaendelea kushirikiana nanyi,” amesema Ngundo, akiongeza kuwa wataendelea kuwaombea washiriki na kudumisha ushirikiano huo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Pendo Mashishanga kutoka Kanisa la AICT Kambarage na Kanon Mazugun kutoka asasi ya kijamii ya PATWA, wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi.

“Tunaishukuru sana timu ya wawezeshaji kutoka Kenya kwa kutupa mafunzo haya. Tunaahidi kwenda kuyafikisha kwa wengine na kufanya kazi kubwa ya kutoa elimu kwa jamii,” wamesema washiriki hao.

Kwa mujibu wa mtaala wa kimataifa wa Safari ya Mpaji-Uzima (Toleo 5.1) uliotolewa na Life International, mafunzo hayo yanajikita katika mada mbalimbali zikiwemo utafiti wa maisha ya mwanadamu, mtazamo wa kibiblia kuhusu uhai, vita vya kiroho, maombi ya maombezi, familia, ujinsia wa kibiblia, uzazi, pamoja na athari na hatua zinazohusiana na utoaji mimba.

Mtaala huo unalenga kuwaandaa viongozi wa Kikristo kimataifa ili waweze kusimamia na kuhamasisha utunzaji wa uhai wa binadamu kwa misingi ya kiimani na kijamii.

Dkt. Meshack Kulwa, Mkurugenzi wa Shirika la Lifeline Cocenselly Centre and Gender Empowerment, akielezea utekelezaji wa mradi wa Safari ya Mpaji Uzima na umuhimu wake kwa jamii.
Mtume Patrick Ngundo, mkufunzi kutoka Nairobi, Kenya, akizungumza na washiriki kuhusu wajibu wa kusambaza elimu waliyoipata kwa jamii.

Collins Kimaro, mkufunzi kutoka Nairobi, Kenya, akizungumza mambo mbalimbali kwa washiriki katika mafunzo ya Safari ya Mpaji Uzima.

 


 SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post