" MAWASILIANO YAREJEA KATIKA DARAJA LA LUBANGALALA; NAIBU WAZIRI KASEKENYA AMPONGEZA MKANDARASI

MAWASILIANO YAREJEA KATIKA DARAJA LA LUBANGALALA; NAIBU WAZIRI KASEKENYA AMPONGEZA MKANDARASI

 

Na Lydia Lugakila-Misalaba Media -Mbeya 

Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya, amempongeza mkandarasi wa kampuni ya Awesome Co. Ltd kwa kujenga daraja la muda kwa haraka katika Mto Lubangalala, wilayani Rungwe mkoani Mbeya.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa daraja hilo, Eng. Kasekenya aliwataka wakandarasi kote nchini kufanya kazi kwa bidii na ubunifu, hasa katika nyakati za dharura, ili kupunguza adha kwa wananchi pale miundombinu ya barabara na madaraja inapoharibika.

“Nakupongeza Mhandisi Grace Frederick kwa kazi nzuri na ya kizalendo uliyoifanya katika kutafuta suluhisho la haraka na kurejesha mawasiliano kati ya wananchi wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya na Ileje mkoani Songwe.

 Tunahitaji wakandarasi wa aina yenu,” amesema Eng. Kasekenya.

Aidha, Naibu Waziri huyo alimpongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha haraka kilichowezesha kurejeshwa kwa mawasiliano katika eneo hilo baada ya daraja kubomoka kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.

“Kurejea kwa mawasiliano kati ya Wilaya za Rungwe na Ileje kutawawezesha wananchi wa mikoa ya Mbeya na Songwe kuendelea na shughuli za kijamii na kiuchumi, hivyo kuchochea maendeleo,” alisisitiza.

Daraja la Lubangalala, linalounganisha mikoa ya Mbeya na Songwe, lilisombwa na mafuriko yaliyotokea kufuatia maporomoko ya mvua mnamo Machi 25 mwaka huu, na kusababisha vifo vya watu 22 pamoja na majeruhi kadhaa.

Kwa upande wake, mkandarasi kutoka Awesome Co. Ltd, Mhandisi Grace Frederick, alishukuru kwa kuaminiwa na kupewa ushirikiano tangu alipoanza ujenzi wa daraja hilo Machi 27.

Naye mmoja wa wananchi wa Rungwe, Emeria Haonga, alisema mafuriko hayo yameleta athari kubwa, ikiwemo kuharibu mazao na kukatiza mawasiliano, lakini aliishukuru Serikali kwa kuchukua hatua za haraka kurejesha hali ya kawaida.









Post a Comment

Previous Post Next Post