" MIKOA YA DAR ES SALAAM, PWANI, ARUSHA, MWANZA NA DODOMA YAONGOZA KWA UWEKEZAJI

MIKOA YA DAR ES SALAAM, PWANI, ARUSHA, MWANZA NA DODOMA YAONGOZA KWA UWEKEZAJI

Waziri Wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Na.Alex Sonna,Mzalendo blog  Dodoma

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji imeendelea kuimarisha utekelezaji wa majukumu yake kwa lengo la kukuza uchumi jumuishi na kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu kupitia Dira ya Taifa ya 2050.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 16,2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri Wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Amesema kuwa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (GN) Namba 407A la tarehe 22 Juni 2023, ofisi hiyo imepewa majukumu 12 muhimu yakiwemo kusimamia sera za uwekezaji, kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje, kuboresha mazingira ya biashara, pamoja na kuratibu maendeleo ya viwanda na maeneo maalum ya kiuchumi.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa majukumu hayo unafanywa kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini ya ofisi hiyo zikiwemo Tume ya Taifa ya Mipango, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA).

Katika hatua nyingine, Waziri Mkumbo amebainisha kuwa maandalizi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050, iliyozinduliwa rasmi Julai 17, 2025 jijini Dodoma na Rais Samia Suluhu Hassan, yamepiga hatua kubwa. Alitaja nyenzo muhimu zilizoandaliwa kuwa ni pamoja na Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV), pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2026/27.

Aidha, Serikali imeandaa mwongozo wa kitaifa wa mipango unaolenga kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali na kuunganisha jitihada za taasisi zote za umma kuanzia ngazi ya taifa hadi halmashauri. Mwongozo huo umeanza kutumika tangu Desemba 2025.

Katika kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo, Waziri amesema Tume ya Taifa ya Mipango imeanzisha mfumo wa kidijitali wa kufuatilia miradi (NPMIS) utakaowezesha ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi kwa wakati halisi na kuongeza uwazi pamoja na uwajibikaji.

Kwa upande wa uwekezaji, taarifa ya kimataifa ya mwaka 2025 inaonesha kuwa Tanzania imeendelea kuvutia uwekezaji wa kigeni, ambapo kiwango cha uwekezaji kilifikia dola za Marekani bilioni 1.72 mwaka 2024 kutoka bilioni 1.34 mwaka 2023, sawa na ukuaji wa asilimia 28.3.

Katika kipindi hicho, Mamlaka ya TISEZA ilisajili miradi mipya 611 yenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani milioni 6,233, inayotarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 100,000. Sekta zilizoongoza ni uzalishaji viwandani, usafirishaji, ujenzi na utalii.

Mikoa iliyoongoza kwa kuvutia uwekezaji ni Dar es Salaam, Pwani , Arusha, Mwanza na Dodoma.

Serikali pia imehimiza matumizi ya tafiti katika upangaji wa maendeleo kwa kuandaa Ajenda ya Taifa ya Utafiti ya mwaka 2026/27–2030/31, itakayosaidia kuboresha ubunifu na kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi wa kisayansi.

Aidha Waziri Mkumbo ametoa wito kwa wizara, taasisi za umma na sekta binafsi kushirikiana kikamilifu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ili kuhakikisha malengo ya Dira 2050 yanafikiwa kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

 
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post