" WAKRISTO WATAKIWA KUSOMA BIBLIA ILI KUJIEPUSHA NA MANABII WA UONGO

WAKRISTO WATAKIWA KUSOMA BIBLIA ILI KUJIEPUSHA NA MANABII WA UONGO


Na Mapuli Kitina Misalaba

 Wakristo wamekumbushwa umuhimu wa kusoma na kuelewa maandiko matakatifu ya Biblia ili kuepuka kupotoshwa na mafundisho ya manabii wa uongo yanayoendelea kujitokeza katika jamii.


Wito huo umetolewa na Askofu Carlton Potts kutoka Texas, Marekani, wakati akihubiri katika ibada ya Jumapili iliyofanyika leo Aprili 12, 2026 Kanisa la AICT Kambarage, mjini Shinyanga.

Askofu Potts amesema baadhi ya watu wamekuwa wakitoa jumbe zisizo sahihi, hivyo ni muhimu kwa waumini kuchunguza kila wanachokisikia kwa kukilinganisha na maandiko matakatifu huku akisisitiza kuwa kila ujumbe unaozua mashaka unapaswa kuthibitishwa kupitia Biblia.

“Maandiko yanasema watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa. Hii ina maana wengi wanaopotoshwa hawana uelewa wa kutosha wa neno la Mungu,” amesema.

Ameongeza kuwa kanisa halijabadilika, bali mabadiliko yapo kwa baadhi ya watu wanaokengeuka kutoka katika misingi ya imani, huku akiwahimiza waumini kuendelea kuwa na matumaini kwa Mungu katika nyakati zote.

Awali akifungua ibada hiyo, Mchungaji wa Kanisa la AICT Kambarage, Charles Lugembe, aliwataka Wakristo kuendelea kumshukuru Mungu kwa amani iliyopo nchini Tanzania, akieleza kuwa hali hiyo imewezesha uhuru wa kuabudu kuendelea kudumu.

Aidha, amewahimiza waumini kuendelea kuliombea taifa ili kudumisha umoja na mshikamano.

Kwa upande wake, Mchungaji mstaafu Amos Ndaki ametumia nafasi hiyo kuwaombea viongozi wa serikali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Waziri Mkuu na viongozi wengine, ili waendelee kuliongoza taifa kwa hekima, amani na utulivu.

Ibada hiyo pia imehudhuriwa na Askofu wa AICT Dayosisi ya Shinyanga, Askofu Zakayo Bugota, huku ikipambwa na uimbaji kutoka kwa kwaya mbalimbali zikiwemo AIC Kambarage Choir, kwaya ya vijana, AIC Shinyanga pamoja na kwaya ya akina mama.

Askofu wa AICT Dayosisi ya Shinyanga, Askofu Zakayo Bugota, akizungumza kwenye ibada ya leo Jumapili katika Kanisa la AICT Kambarage. 

Mchungaji wa Kanisa la AICT Kambarage, Charles Lugembe, akiongozi ibada ya leo Jumapili.

Mchungaji wa Kanisa la AICT Kambarage, Charles Lugembe, akiongozi ibada ya leo Jumapili.







 

Post a Comment

Previous Post Next Post