" MWALIMU AUWAWA KIKATILI SUMBAWANGA

MWALIMU AUWAWA KIKATILI SUMBAWANGA




Jeshi la Polisi Mkoa wa Rukwa limewakamata watuhumiwa (25) kwa tuhuma za kuhusika katika tukio la mauaji ya Henry Shubati Myuwanga (50), Mwalimu wa Shule ya Msingi Wema Mkoani Songwe.

Tukio hilo la mauaji lilitokea tarehe 04 Aprili, 2026 majira ya saa 02:30 usiku katika Kijiji cha Kilyamatundu, Wilaya ya Sumbawanga.

Marehemu alifika kijijini hapo siku hiyo akitokea Mlowo, Mkoa wa Songwe kwa lengo la kuuza sabuni za maji anazozitengeneza, biashara ambayo amekuwa akiifanya mara kwa mara kijijini hapo anapokuwa na muda wa kufanya hivyo.

Chanzo cha tukio hilo kilitokana na kutokukubaliana bei ya sabuni kati ya mwalimu (marehemu) na kijana mmoja muuza duka kijijini hapo aitwaye Cleuben Simchimba ambaye amekimbia tunaendelea kumtafuta.

Kufuatia hali hiyo, kijana huyo aliamua kufanya kitendo kiovu cha kupiga kelele na kumtuhumu marehemu kuwa amemshika begani na kwamba nyeti zake zimepotea.

Kutokana na kelele za kijana huyo, wananchi walikusanyika na kuanza kumshambulia mwalimu huyo kwa kumpiga mawe na baadaye kuchoma moto mwili wake. Pamoja na watuhumiwa 25 kukamatwa msako mkali bado unaendelea ili kuhakikisha wale wote waliohusika kumshambulia mwalimu wanakamatwa ili hatua zingine kwa kujibu wa sheria zichukuliwe.

Jeshi la Polisi linaonya vikali vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi, kwani ni kinyume cha sheria na vinasababisha madhara makubwa, ikiwemo kupoteza maisha ya watu wasio na hatia kama huyu mwalimu alivyouawa baada ya kushindwana bei na kusingiziwa kuiba nyeti.

Vilevile tunawahimiza wananchi kupuuza na kutoeneza taarifa za uzushi zinazochochea hofu na taharuki na madhara mengine kwa jamii, hususan zile zinazohusiana na madai ya wizi wa viungo nyeti vya mwili wa binadamu kwa njia za kishirikina.

Jeshi la Polisi linaendelea kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi katika kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kudumisha amani na usalama wa jamii.

Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa

Post a Comment

Previous Post Next Post