" UFAFANUZI KUHUSU WATU KUPOTEZA SEHEMU ZA SIRI

UFAFANUZI KUHUSU WATU KUPOTEZA SEHEMU ZA SIRI






TAARIFA KWA UMMA

Hivi karibuni kumejitokeza tabia za baadhi ya watu na mashabiki wao kuwatuhumu watu wengine kuwa, wamewashika mabegani watu fulani na matokeo yake sehemu zao za siri zimetoweka.

Tabia hizo zinazoongozwa na imani za kishirikina zilianza kuibuka maeneo ya Tunduma Mkoa wa Songwe Aprili 1,2026 na kusababisha vifo vya watu watano na wengine wawili kujeruhiwa na wamelazwa hospitali kwa matibabu.

Tabia hiyo pia imejitokeza Aprili 3,2026 huko Makongolosi na Mtaa wa Maendeleo Jijini Mbeya ambapo watu wawili walishambuliwa na kujeruhiwa na hivi sasa wanaendelea na matibabu hospitalini.

Aidha, matukio kama hayo yametokea eneo la Kimara Mwisho na Mbezi Shule Jijini Dar es Salaam Aprili 3,2024 majira ya jioni ambapo watu wawili wanaume nao walituhumiwa kuwa, wamewagusa watu mabegani na matokeo yake sehemu zao za siri zikatoweka.

Leo Aprili 4,2026 katika Jiji la Mbeya kumejitokeza tena matukio mengine mawili yaliyotokea eneo la Kabwe Wilaya ya Mbeya Mjini na Double J Kalumbulu Wilaya ya Kyela ambapo watu wawili wamajeruhiwa kwa tuhuma hizo hizo za uzushi ambapo mmoja wa anayedai kufanyiwa hivyo alipofanyiwa uchunguzi na Madaktari sehemu zake zilikutwa zipo na hazina tatizo lolote.

Tabia hizi zinazoongozwa na imani za kishirikina, mihemko ya kishabiki na malengo ambayo hayaja bainika hazina ukweli wowote kwani wanaodaiwa kuguswa bega na sehemu zao za siri kutoweka walipokaguliwa sehemu zao za siri zilikutwa zikiwa maeneo yake kama kawaida na maeneo mengine anayedaiwa kufanyiwa hivyo alipotafutwa hakuonekana na wala waliokuwa wana shabikia na kuwa wazungumzaji wakuu wakielezea uzushi huo walipotakiwa kumwonyesha aliyechukuliwa sehemu zake za siri hawakuweza kumwonyesha wala kutoa uthibitisho wa alichokuwa anaeleza kwa mbwembwe na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii.

Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa wote wale wanaoendekeza uzushi na tabia hizi zinazo ongozwa na imani za kishirikina zilizopitwa na wakati katika dunia hii ya sayansi na teknolojia kuziacha mara moja na yeyote atakaye bainika kuziendekeza pamoja na mashabiki wao watakamatwa kwa hatua zingine za kisheria kwa sababu tabia hizo za uzushi zinahatarisha maisha ya watu kama ambavyo imeshasababisha vifo vya watu watano na majeruhi.

Aidha, Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza walioandaa na kuzusha uvumi huu ni akina nani na malengo yao ni nini.

Imetolewa na;
Msemaji wa Jeshi la Polisi
Makao Makuu ya Polisi
Dodoma,Tanzania

Post a Comment

Previous Post Next Post