" THTU YATAKA MABORESHO YA UTAWALA BORA KUFANIKISHA DIRA 2050

THTU YATAKA MABORESHO YA UTAWALA BORA KUFANIKISHA DIRA 2050

Na Mwandishi wetu, Dodoma

Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) kimeitaka Serikali kuimarisha utawala bora na mifumo ya kisheria ili kuhakikisha utekelezaji wenye mafanikio wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Hayo yameelezwa katika andiko la ushauri kuhusu siasa na sheria lililowasilishwa serikalini, likilenga kuchambua changamoto za kisiasa na kisheria zinazoweza kuathiri maendeleo ya taifa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa THTU Taifa, Dk. Paul Loisulie, utawala bora ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu na unapaswa kuimarishwa katika ngazi zote.

Alisema pamoja na Tanzania kuwa na mfumo mzuri wa kikatiba na kisheria, bado kuna changamoto ya utekelezaji wa sheria hizo kwa vitendo, hali inayodhoofisha uwajibikaji na ufanisi wa taasisi za umma.

“Ni muhimu kuziba pengo la utekelezaji wa sera na sheria ili kuhakikisha haki, uwazi na ushiriki wa wananchi vinaimarika,” alisema.

THTU imebainisha changamoto mbalimbali ikiwemo masuala ya haki za binadamu, uhuru wa taasisi, ushiriki mdogo wa wananchi na uwepo wa rushwa ya kimfumo.

Katika mapendekezo yake, chama hicho kimeitaka Serikali kufanya marekebisho ya kisheria na kisera, kuimarisha taasisi za umma, pamoja na kuongeza ushiriki wa wananchi katika maamuzi ya maendeleo.

Chama hicho kimesisitiza kuwa bila utawala bora, utekelezaji wa Dira 2050 hautaweza kufikiwa kwa ufanisi.

Post a Comment

Previous Post Next Post