IMEELEZWA kuwa kila raia na mkazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anao wajibu wa kipekee wa kugeuka kuwa dalali wa amani na mshikamano wa kitaifa ili kuponya majeraha yaliyotokana na matukio ya uvunjifu wa amani ya Oktoba 29 2025.
Wito huu umetolewa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) ikiwa ni sehemu ya wajibu wao wa kisomi kwa jamii katika kutoa tafakuri juu ya wasilisho la ripoti ya Tume ya Rais iliyokuwa ikichunguza machafuko hayo.
Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa UDASA, Elgidius Edgar Bwinabona Ichumbaki amesisitiza kuwa msingi wa utulivu wa nchi unategemea dhamira ya dhati ya kila mtu katika kulinda haki na usawa huku akibainisha kuwa amani si jambo la kuachiwa serikali na vyombo vyake pekee.
Wanataaluma hao wameeleza kuwa ingawa ripoti kamili ya Tume ya Jaji Mohamed Chande Othman bado haijawekwa hadharani tangu iwasilishwe kwa Rais Samia Suluhu Hassan mnamo Aprili 24 mwaka 2026 wamefanya uchambuzi wa kina kupitia wasilisho la picha mjongeo la mwenyekiti huyo.
Katika jicho la kitaaluma UDASA imebaini mambo zaidi ya hamsini ambayo ni kero za msingi kwa wananchi na vyanzo vya machafuko vilivyopelekea vifo na uharibifu wa mali wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka 2025.
Wasomi hao wamekiri kuwajibika kwa upande wao kwa kushindwa kutimiza takwa la uhuru wa kitaaluma na uwajibikaji wa kijamii hapo awali jambo ambalo limechangia sintofahamu iliyojitokeza nchini.
Katika mfululizo wa kero hizo UDASA imebainisha kuwa kukosekana kwa Katiba Mpya inayokidhi matakwa ya wananchi na Tume ya Uchaguzi kutokuwa huru ni miongoni mwa sababu kuu zilizozalisha hasira miongoni mwa wadau wa siasa na wafuasi wa vyama vya upinzani.
Aidha jumuiya hiyo imemulika mapungufu ya kiutendaji katika vyombo vya dola ikitaja Jeshi la Polisi kutotumia haki na kutumia nguvu kupita kiasi pamoja na Idara ya Usalama wa Taifa kushindwa kutimiza wajibu wake kikamilifu.
Aidha taarifa hiyo imegusia hali ya watu kutekwa na kupotezwana kueleza hali hiyo kama tishio kubwa kwa haki ya kuishi jambo ambalo limepunguza imani ya wananchi kwa mifumo ya kisheria na kiutawala.
Uchambuzi huo wa UDASA pia umejikita katika hali ya kiuchumi na kijamii ambapo ukosefu wa ajira kwa vijana na kutoridhishwa kwa wafanyakazi wa sekta ya umma kutokana na mazingira magumu ya kazi na mishahara midogo kumeongeza msongo wa mawazo na matatizo ya afya ya akili.
Wasomi hao wameeleza kuwa uongo wa wazi unaotolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na serikali pamoja na kiburi cha watumishi wa umma kimechangia mmomonyoko wa uzalendo. Pia wameonya kuhusu ubadhirifu wa mali za umma na maisha ya anasa ya baadhi ya viongozi huku wananchi wa kawaida wakikabiliwa na utitiri wa kodi na umaskini uliokithiri.
Ili kuepuka machafuko mengine siku za usoni UDASA imetaka serikali kusikiliza ushauri wa wataalamu na busara za viongozi wa dini pamoja na kufanya maboresho makubwa katika mifumo ya kidemokrasia na uwajibikaji.
Wamesisitiza kuwa mbinu za sasa za kutatua kero za wananchi zimepitwa na wakati na haziendani na kasi ya vijana wa kizazi kipya maarufu kama Gen-Z.
Katika tafakuri hiyo Udasa pia imesisitiza kuwa uponyaji wa mioyo ya Watanzania na ulinzi wa amani ya kudumu utapatikana tu pale serikali itakapofanyia kazi mambo hayo kwa ukamilifu wake.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment