" USAFI SOKO LA MNARA WA VODA WAZUA MALALAMIKO KWA WAJASIRIAMALI

USAFI SOKO LA MNARA WA VODA WAZUA MALALAMIKO KWA WAJASIRIAMALI

 Na Edington Mukiza Ezron, Misalaba Media

Baadhi ya wajasiriamali wa Soko la Mnara wa Voda wamelalamikia hali ya usafi katika soko hilo, wakiiomba serikali kuajiri wafanyakazi maalum wa kufanya usafi ili kuboresha mazingira na kupunguza usumbufu unaowakabili.

Akizungumza na Misalaba Media katika soko hilo, Irene Pascal amesema licha ya wajasiriamali kuchangia fedha za ukusanyaji taka, bado hali ya usafi hairidhishi, hivyo kuna haja ya kuwepo kwa mfumo rasmi wa usimamizi wa usafi kama ilivyo katika masoko mengine.

Aidha, ameeleza kuwa soko hilo linakabiliwa na upungufu wa vyoo, hali inayoweza kuchochea magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu, na kuomba mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kujenga miundombinu hiyo muhimu.

Wajasiriamali hao pia wamebainisha kuwa baadhi ya wafanyabiashara hawazingatii usafi wa mazingira yao, jambo linalochangia kuzorota kwa hali ya soko. Wamewataka wenzao kushirikiana katika kudumisha usafi ili kulinda afya zao na kuvutia wateja.

Kwa upande wake, Katibu wa Soko hilo, Samson Marwa, amekiri kuwepo kwa changamoto hizo na kuziomba mamlaka za afya kutembelea soko hilo mara kwa mara kwa ajili ya kutoa elimu na kufanya tathmini ya hali ya usafi.

Hata hivyo, wamezitaka mamlaka husika kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wale wanaokiuka taratibu za usafi ili kukomesha tatizo hilo na kuboresha mazingira ya biashara.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post